Kauli hiyo ya serikali ilitolewa baada ya gazeti hili toleo namba 1083 la Machi 6-12, 2018 kueleza kuwa, kuna baadhi ya Watanzania walinyongwa nchini China kutokana na kukamatwa na kukutwa na makosa ya kuwa na dawa za kulevya.
Msajili wa Magazeti, Patrick Kipangula alipokutana na wahariri wa gazeti hili alisema amepata taarifa kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini China kuwa nchi hiyo haijanyonga Mtanzania kutokana na kukutwa na madawa ya kulevya.
“Afisa mmoja wa ubalozi wetu nchini China alisema nchi hiyo haijanyonga Mtanzania kutokana na makosa ya kukutwa na madawa ya kulevya,” alisema Kipangula.
Hata hivyo, serikali iliwahi kusema kuwa Watanzania 408 wanatumikia vifungo nje ya nchi na wengine kukabiliwa na adhabu ya kifo baada ya kusafirisha dawa za kulevya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Akizungumzia Watanzania waliokamatwa kwa dawa hizo, Mahiga alisema kuwa wanakabiliwa na adhabu hizo katika magereza mbalimbali duniani baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kujihusisha na biashara haramu.
Mahinga alitaja idadi yao na nchi ambazo wanashikiliwa kuwa ni Brazil (41), China (266), Iran (68), India (9), Nepal (4), Oman (3), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3).
Hata hivyo, gazeti hili linawaomba radhi wale wote walioguswa na kukerwa habari ambayo tuliiandika ikiwa na kichwa cha ‘WAUZA UNGA WANAVYONYONGWA CHINA INATISHA!’ wakiwemo ndugu wa Sandra Khan (Binti Kiziwi) pichani.
SOMA PIA: Nafasi za Ajira East African Community