Mbunge wa Geita Vijijini Joseph msukuma ameitaka serikali iwafukuze wabunge wenye elimu ya darasa la 7, iwapo haitawarudisha kazini walimu na watendaji wa serikali waliokuwa na elimu ya darasa la saba.
Msukuma ameyasema hayo Bungeni leo alipokuwa akichangia hotuba ya ofisi ya Waziri Mkuu, na kwamba wakishaondolewa warudishwe kama wabunge wa viti maalum ili wawatetee darasa la saba wenzao.
“Wabunge wenzangu wa CCM tutoe tamko la kuwarudisha hawa watendaji na sio kuwalipa, na kama serikali itakaidi, na humu ndani kuna wabunge darasa la saba zaidi ya mia, na sio la saba tu, hata waliofeli form four, wenye vyeti havieleweki wapo humu ndani, ninaomba sana serikali kama hamuwezi kuwarudisha hawa watendaji, na sisi wabunge wa darasa la saba humu ndani mtufukuze, sioni sababu hata ya wabunge wa darasa la saba kuwa humu ndani, ni bora katiba ikatuondoa humu, mturudishe kwa viti maalum kwa sababu na sisi tuko wengi wa darasa la saba”, amesema Mbunge Msukuma.
Mbunge Msukuma ameendelea kwa kusema kwamba kitendo cha serikali kufukuza watendaji wa serikali ambao wana elimu ya darasa la saba sio sahihi na sio haki, kwani wao ndio watendaji wazuri wa kazi kuliko wale wenye elimu kubwa.
“Nashangaa ni kwa nini wamewafukuza watendaji wa vijiji wa darasa la saba, wanataka hizi nafasi za watu wa darasa la saba wapewe watu wa vyuo vikuu, ni kijiji gani mmepeleka mtendaji 'graduate' aliyeweza kufanya kazi akawazidi darasa la saba, tumefukuza madereva, mnataka watoto wenu wanaosoma nje mpaka vyo vikuu ndio wakawe madereva, mnamfukuza mtu amebakiza miaka miwili ya ustaafu, hamfanyi haki”, amesema Mbunge Joseph Msukuma.