Serikali imetaifisha dhahabu ya mabilioni ya shilingi na magari ya kifahari kutokana na wahusika wake kukamatwa na kuhukumiwa kwa makosa ya rushwa katika mwaka huu wa fedha.
Pia imetaifisha, pikipiki, mafuta, mashine za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa linatumika kusafirisha meno ya tembo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, aliyasema hayo jana alipowasilisha bungeni mjini hapa hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.
Alibainisha kuwa katika mwaka huu wa fedha, mali zilizotaifishwa kwa ujumla wake zinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 5.685.
Waziri huyo alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilipokea majalada 683 ya tuhuma za rushwa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru).
Prof. Kabudi alisema kati ya hayo, majalada 288 yaliandaliwa hati za mashtaka na 275 yalirudishwa Takukuru kwa uchunguzi zaidi.
Alisema majalada 115 yako katika hatua mbalimbali yakifanyiwa kazi na mengine matano yalifungwa.
"Washtakiwa waliotiwa hatiani walipewa adhabu mbalimbali zikiwamo vifungo, faini na mali kutaifishwa ambapo jumla ya Sh. bilioni 4.484 zilitozwa kama faini kutoka kwa washtakiwa," alisema na kuongeza:
"Mali zilizotaifishwa ni pamoja na kilogramu 24.5 za dhahabu zenye thamani ya Sh. bilioni 2.012 na fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya Sh.milioni 908.092.
"Mali zingine zilizotaifishwa ni magari matano ya kifahari aina ya Range Rover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba, pikipiki 34, mafuta, mashine za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa linasarifirisha meno ya tembo."
Prof. Kabudi alisema mwaka huu wa fedha pia mali za vyama vya ushirika vya Mwanza (Nyanza Cooperative Union) na Shinyanga (Shirecu) zikiwamo nyumba, viwanja na viwanda, zimerejeshwa serikalini kutoka mikononi mwa watu ambao walizichukua bila kufuata utaribu wa kisheria.
Waziri huyo pia alisema mwaka huu wa fedha kulikuwa na mashauri sita yanayohusu ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliyoshughulikiwa.
Alisema kuwa kati yake, mashauri manne yalikamilika kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu za kifungo cha kati ya miaka minne hadi 20 na mashauri mawili yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa.