Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine sita wa chama hicho wamerejea uraiani jana baada ya kutimiza masharti ya dhamana, huku Jamhuri ikiomba kesi ya uchochezi inayowakabili isikilizwe haraka kwa kuwa ushahidi umekamilika.
Wengine waliopata dhamana baada ya kusota mahabusu kwa siku tano ni Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; na mhazini wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Esther Matiko.
Kiongozi mwingine aliyeachiwa kwa dhamana baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa na wenzake ni mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee aliyekamatwa na Polisi Jumapili usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Afrika Kusini.
Baada ya kusomewa mashtaka ya uchochezi na uasi, Jamhuri ilipinga dhamana ya Mdee ombi lililokataliwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Machi 27, viongozi hao isipokuwa Mdee, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka manane yakiwamo ya kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Kati ya makosa hayo, mawili yanawakabili wote sita ambayo ni kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali Februari 16 wakiwa Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni.
Masharti ya dhamana waliyotimizwa ni kila mshtakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni; kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka uongozi wa mtaa au kijiji; nakala za vitambulisho vyao; na kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi kila Ijumaa.
Walifikishwa Kisutu jana saa mbili asubuhi na walisubiri hadi saa 5:47 asubuhi Hakimu Mashauri alipoingia mahakamani.
Wakati kesi ikiendelea, idadi kubwa ya wanachama wa Chadema waliojitokeza nje ya uzio wa Mahakama wakiimba nyimbo kutaka viongozi hao waachiwe, walitawanywa na polisi kwa kumwagiwa maji ya kuwasha na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema 26 wanashikiliwa akiwamo mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Baada ya Hakimu Mashauri kuingia mahakamani, upande wa mashtaka uliomba kurekebisha hati ya mashtaka ili kumwongeza Mdee katika kesi hiyo. Pia, uliomba kuwasomea washtakiwa makosa upya lakini mawakili wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala walipinga wakiomba Mahakama itekeleze kwanza amri ya masharti ya dhamana kwa washtakiwa wa awali. Mahakama ilikubali ombi hilo, hivyo wadhamini wa washtakiwa waliwasilisha vielelezo vyao vya dhamana ambavyo baada ya kukaguliwa na kujiridhisha walidhaminiwa.
Dhamana ya Mdee yapingwa
Baada ya hilo, Mdee alipandishwa kizimbani na washtakiwa wote walisomewa upya mashtaka ambayo walikana kuyatenda.
Kibatala aliiomba Mdee apewe dhamana kwa masharti kama yaliyotolewa kwa washtakiwa wengine kwa kuzingatia msingi wa kisheria wa uamuzi wa mashauri yanayofanana lakini Jamhuri ilipinga ikidai alishindwa kutekeleza masharti ya dhamana ya polisi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alisema kabla ya kufikishwa mahakamani, Mdee alipewa dhamana polisi ambayo hakukidhi masharti yake yaliyomtaka kuripoti mara moja kwa wiki lakini hakuhudhuria mara tatu mfululizo Machi 15, 22 na 29.
Wakili mwingine wa Serikali Faraja Nchimbi aliiomba Mahakama kama itaona ni lazima kumpa dhamana, izingatie vigezo vya kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na wadhamini, kuwasilisha polisi hati za kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali.
Kibatala akijibu hoja hizo za Jamhuri alisema ni za kufikirika, kwamba mawakili si maofisa wapelelezi, wakamataji wala waliompa dhamana hivyo wanayoyasema ni uvumi.
Hakimu Mashauri alitupilia mbali pingamizi la dhamana dhidi ya Mdee akisema hakuna sheria inayoeleza kuwa mshtakiwa akiruka dhamana ya polisi na mahakamani anyimwe dhamana kwa kuwa hizo ni taasisi mbili tofauti.
Ombi kesi kusikilizwa mfululizo
Baada ya uamuzi huo, Nchimbi aliwasilisha ombi kuwa Mahakama iruhusu kesi isikilizwe haraka akisema upelelezi umekamilika.
Aliomba usikilizwaji wa awali ufanyike leo mchana ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali ya kesi na Mahakama ipange tarehe ya kuanza usikilizwaji rasmi wa ushahidi. Alisema msingi wa ombi hilo ni kutokana na ukweli kwamba washtakiwa wengi ni wabunge na kwa nafasi zao kesi hiyo inavuta hisia za watu wengi.
Kibatala alipinga ombi hilo akisema yeye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi na kwamba leo atakuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na kesho atakuwa na kesi nyingine.
Alisema pia atakuwa na vikao na mkutano wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) jijini Arusha, hivyo aliomba usikilizwaji wa awali ufanyike Aprili 16 ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Mashauri.
Baada ya kutoka mahakamani, Mbowe alisema ameona mengi mahabusu na atapanga siku ya kuyaeleza na kutoa taarifa ya kesi inayowakabili.