Mahakama Kuu imeelezwa kuwa simu, laini na pikipiki zilizotumika katika mipango ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya, zilinunuliwa kwa maelekezo ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed.
Pia, mahakama chini ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, ilielezwa kuwa baada ya kumkamata Sharifu aliwataja watu wengine wawili ambao ni Shaibu Mredii (mshtakiwa wa pili) na Joseph Chussa (sio miongoni mwa washtakiwa wa kesi hiyo kwa sasa).
Hayo yamo katika ushahidi wa shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, mkaguzi wa Polisi, Damian Chilumba, aliyedai ujumbe wa mwisho (SMS) uliotumwa kwenye simu ya marehemu, saa chache kabla ya kuuawa Agosti 7, 2013 uliwasaidia makachero kuwanasa watuhumiwa.
Shahidi huyo wa Serikali, jana alipata fursa ya kusoma maelezo ya mashahidi watatu, Hamisa Kassim, Evelyne Munis na Shaaban Mahmoud ambao wametoweka na hawajulikani walipo.
Chilumba ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya mawasiliano ya kimtandao (Cyber), alidai mahakamani jana kuwa timu yake ndiyo iliyobaini uwapo wa namba ya mwisho iliyowasiliana na marehemu.
Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai baada ya kufanikiwa kuondoa neno la siri katika simu za marehemu, walikuta SMS mbili.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kufungua simu mojawapo ya marehemu, walikuta SMS hizo zikiwa zimetumwa kupitia namba ya mtandao wa Airtel siku moja kabla ya mauaji na siku ya mauaji.
“Ujumbe wa kwanza ulitumwa tarehe 6/8/2013 ukimjulisha (marehemu) kuwa ‘nina riziki’ na ujumbe wa tarehe 7/8/2013 saa nne au saa tano hivi ulisema niko Kia nakusubiri hapa,” alidai shahidi huyo na kuongeza:
“Tulianza kufuatilia ujumbe huo (wa tarehe 7/8.2013) ambao ndiyo ulikuwa wa mwisho kwenye simu ya marehemu na saa chache baadaye akauawa. Tuliandika barua Airtel kupata taarifa zake.”
Katika barua hiyo, shahidi huyo alidai waliiomba kampuni ya Airtel kuwapa taarifa mmiliki wa laini hiyo ya simu, ilikosajiliwa na kwa wakati huo ilikuwa ikisomeka eneo gani.
Alidai kuwa majibu ya Airtel yalionyesha kuwa laini hiyo ilikuwa imesajiliwa Arusha Agosti 3, 2013 kwa jina la Motii Mongululu lakini wakati huo haikuwa tena hewani.
“Walituambia baada ya kusajiliwa, laini hiyo ilifanya mawasiliano na namba nne tu na wakatuambia iliwahi kuchomekwa kwenye handset (simu) ambayo inatumia namba nyingine,” alidai na kuongeza:
“Tulifanikiwa kumkamata dada mmoja pale Arusha kituo kikuu cha mabasi anaitwa Hamisa (Kassim), ambaye ndiye mwenye hiyo namba, ambaye alikumbuka kusajili line kwa jina la Motii Mongululu.”
Hata hivyo, shahidi huyo alidai katika mahojiano, Hamisa aliwaeleza kuwa alisajili laini hiyo kwa maelekezo ya wakala mwenzake aliyemtaja kuwa ni Aneth Shija ambaye naye alikamatwa.
“Aneth alikiri ndiye aliyempa maelekezo Hamisa kusajili hiyo laini na nyingine mbili na kwamba, alizisajili kwa maelekezo ya mtu aliyemtaja kuwa ni Adam ambaye ni kijana wa kimasai,” alieleza.
Shahidi huyo alidai kupitia kwa Aneth walifanikiwa kupata namba ya Adam ambaye alikamatwa Mirerani, lakini naye akadai aliagizwa na mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu kusajili laini hizo.
Mkaguzi huyo wa polisi aliieleza mahakama kuwa baada ya Mangu kukamatwa na kuhojiwa, alikiri kusajili laini hizo za simu lakini naye akadai kuwa alitumwa na mshtakiwa wa kwanza, Sharifu.
“Alituambia maelekezo ya kusajili laini na kununua simu alipewa na bosi wake aliyemtaja kuwa ni Sharifu Mohamed. Alitueleza kuwa kwa ufahamu wake, yote yalikuwa ni maandalizi ya mauaji.
“Siku hiyo hiyo tulimkamata Sharifu nyumbani kwake na katika mahojiano ya awali alimtambua Mussa kama mfanyakazi wake na kukiri vitu vyote vilivyonunuliwa naye vilikuwa maelekezo yake,” alieleza.
Alivyomtaja Chusa
Shahidi huyo ambaye sasa yuko Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, alitaja vitu ambavyo Sharifu aliwaelekeza Mangu na Adamu wavinunue ni simu mpya, laini za simu na pikipiki mbili mpya.
“Kutoka kwa Sharifu akatuongezea watu wengine wawili ambao ni Shaibu Mredii (mshtakiwa wa pili) na Joseph Chussa (si miongoni mwa washtakiwa wa kesi hiyo kwa sasa),” alidai shahidi huyo.
Chussa alikuwa miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo kwenye hatua za awali, lakini mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kwa kutumia mamlaka yake, alimfutia mashtaka hayo Aprili 17, 2014.
Shahidi huyo alieleza kuwa Mredii alikamatwa na polisi akiwa Mirerani na kazi ya kuwatafuta washtakiwa wengine katika kesi hiyo iliendelea na alikamatwa mshtakiwa wa nne, Jalila Zuberi.
Aliieleza mahakama kuwa timu mbalimbali za upelelezi ziliendelea na kazi ya kuwasaka watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata washtakiwa Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Majeshi.
Mkaguzi huyo wa polisi alidai baada ya kukamatwa kwa Karim na Sadick wilayani Kaliua mkoani Tabora, Sadick anadaiwa kuelekeza mahali alipoficha bunduki iliyotumika katika mauaji hayo.
Timu ya makachero ikiongozwa na mkuu wa upelelezi (RCO) Mkoa Kilimanjaro, Ramdhan Ng’anzi walikwenda Sanya Juu wilayani Siha na kufanikiwa kuipata bunduki hiyo.
Shahidi huyo alidai ndiye aliyewapeleka washtakiwa Karim na Sadick ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali Arusha kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli za vinasaba (DNA) na jaketi lililopatikana eneo la tukio.
Pia, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa yeye na shahidi wa nane, mkaguzi msaidizi wa polisi, Herman Mutungi, ndio waliopeleka bunduki hiyo kwa mtaalamu wa milipuko jijini Dar es Salaam.
Akingozwa na Chavulla ambaye kwa jana alisaidiana na Ignas Mwinuka, shahidi huyo alidai ndiye aliyeandika maelezo ya mashahidi watatu ambao hawapatikani.
Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee maelezo ya mashahidi hao, Hamisa Kassim, Evelyne Munis na Shaaban Mahmoud, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama na akapata fursa ya kuyasoma.
Maelezo ya Hamisa
Katika maelezo yake, Hamisa aliyekuwa wakala wa kusajili laini za simu, alieleza kuwa rafiki yake aitwaye Aneth Shija, alimweleza kuwa kuna kijana wa kimasai aitwaye Adam anamtaka kimapenzi.
“Huyo Aneth mara nyingi anasajili laini zake bila kufuata utaratibu, mara ya mwisho alisajili laini tatu yaani tarehe 5/8/2013 na 6/8/2013. Mtu anayetaka kusajili laini lazima awe na kitambulisho.
“Nakumbuka 5/8/2013 alikuja Adam akiwa na mwenzake wakiongea lugha ya kimasai lakini Aneth hakuwapo na alikuwa amemwachia ofisi yake dada mmoja anaitwa Eva (Evelyne Munisi),” anaeleza.
Kulingana na maelezo hayo, Hamisa anadai alimuona Eva anajaza fomu kwa ajili ya kumsajilia laini huyo Adam, lakini hakukuwa na kitambulisho ila hazikupokea vocha.
“Kutokana na matatizo hayo, huyo Eva alikuja kwangu nikawaambia ni tatizo tu la mtandao. Waliondoka na siku iliyofuata walikuja tena na kupewa zile laini zikiwa zinafanya kazi,” alidai.
Maelezo ya Evelyne
Akisoma maelezo ya Evelyne, shahidi huyo alimnukuu akisema alifahamiana na Aneth alipokwenda siku moja kusajili laini yake ya Tigo katika kituo hicho cha mabasi Arusha na wakawa marafiki.
“Siku moja tarehe 3/8/2013 nikiwa Moshi niliona simu ya Aneth akinipigia nikamwambia niko njiani nakwenda Arusha. Nilipofika Arusha aliniomba nimsaidie kubaki kwenye ofisi yake,” anaeleza.
Evelyne ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Nairobi Institute cha jijini Arusha, anadai siku moja Aneth alimpigia simu na kumweleza kuna kijana atakuja amsajilie simu kwa jina la Motii Mongululu.
“Nilimpelekea Hamisa anisaidie kumsajilia hizo laini. Alikuja Adam na kuchukua hizo laini mbili nilizozisajili kwa jina la Motii Mongululu, ingawa niliona alishasajili tena kwa jina la Motii Ndoole.
“Tarehe 6/8/2013, Aneth alinipigia tena simu akaniambia nichukue laini nisajili kwa jina la John Francis. Nilimpelekea Hamisa nikamwambia Aneth kasema Adam atakuja kuichukua,” alieleza.
Katika maelezo ya shahidi mwingine, Shaaban Mohamed, alinukuliwa akisema siku asiyoifahamu Agosti 2013, alifika nyumbani kwake eneo la Bomang’ombe, mtu aliyemtaja kwa jina la Said Jabir.
Shaaban anadai Said alikuja na pikipiki mpya aina ya King Lion nyeusi na alipomuuliza kama amenunua, alimweleza ni ya kaka yake ambaye ni mshtakiwa wa sita, Sadik Jabir.
Hata hivyo, anadai baada ya siku kadhaa kupita, Said alikuja na makachero wa Polisi wakiitaka pikipiki hiyo na alimweleza akaichukue mahali alipokuwa ameipaki ndani ya nyumba yake.
Mkaguzi huyo wa polisi katika ushahidi wake, alidai yeye ndiye aliyekabidhiwa pikipiki hiyo na kurudi nayo Moshi, alimkabidhi Inspekta Samwel Maimu aliyekuwa mtunza vielelezo.
Kesi hiyo itaendelea leo kwa jopo la mawakili wa utetezi linaloundwa na Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu, watakapopata nafasi ya kumdodosa shahidi huyo.
Shaidi Atema Cheche Mahakamani Kesi ya Bilionea Msuya...... Afunguka Siri Nzito Kuhusu Simu, Laini na Pikipiki Zilizotumika Katika Mipango ya Mauaji
April 25, 2018
Tags