Awali habari zilidai kwamba Wema alishindwa kuhudhuria kwenye msiba huo kutokana na kwamba yeye na marehemu Masogange walikuwa na bifu kali na hawakuwahi kupatana.
“Unajua Wema na Masogange walikuwa hawaivi, sasa inawezekana ndiyo maana hajaonekana msibani. Au ana sababu nyingine? Mimi kwa kweli nimeshangaa kutomuona,” alisikika akisema mmoja wa waombolezaji aliyekuwa amefika katika Viwanja vya Leaders jijini Dar kuuaga mwili wa Masogange.
SIRI YAFICHUKA
Kutokana na gumzo la Wema kuutosa msiba huo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta kwa njia ya simu yake ya mkononi lakini iliita bila kupokelewa. Baada ya kutopokelewa, gazeti hili liliamua kumtafuta meneja wake, Neema Ndepanya ambaye alitoa siri ya Wema kutohudhuria msibani hapo ambapo alisema mwanadada huyo alipatwa na tumbo la ghafla ambalo lilimzuia kutoka kwenda popote.
“Wema alikuwa na nia ya kufika msibani kabisa na alikuwa ameshajiandaa lakini ilishindikana baada ya kuugua tumbo la ghafla ikabidi aahirishe tu, pia Mbeya alishindwa kusafiri maana Jumatatu ambayo ndiyo mazishi ya Masogange alikuwa anatakiwa kuhudhuria mahakamani kwenye kesi yake inayoendelea,” alisema Neema.
Masogange alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini Dar na mwili wake kuagwa Aprili 22 katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni na kusafirishwa nyumbani kwao Mbeya kwa mazishi yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.
STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko.