Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa sababu za kiongozi wa upinzani bungeni kutokuwa na gari lake linalohudumiwa na Bunge kuwa ni kutokana na dereva wake kustaafu.
Spika Ndugai amesema dereva wa gari hilo alistaafu katika kipindi cha Bunge la Tisa lakini aliendelea kuwa na mkataba kwa vipindi vyote hivyo sasa Bunge limeona umri wake umekuwa mkubwa zaidi.
Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Aprili 17 wakati anatolewa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa April 12 na Mbunge Ukonga(Chadema), Mwita Waitara kuhusu watumishi wa upinzani walioondolewa.
Spika Ndugai amekiri kuwa hawapo baada ya kumaliza muda wao wa mkataba tangu Desemba mwaka jana na akasema kwa sasa wanaendelea kutazama na watalizungumza kwani linahitaji mjadala mpana hivyo akaomba upinzani wasigomee kusoma hotuba za upinzani.
Kiongozi huyo amesema mbali na watumishi wanne wa upinzani, lakini Bunge limewafungashia virago watumishi watano wa upande wa CCM hivyo nao hawana watendaji hadi Bunge litakapoamua vinginevyo kutokana na mambo ya kiusalama.