NEEMA imezidi kumfungikia mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Samatta anayekipiga katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelegiji baada ya klabu tatu za England kumuwania.
Samatta aliyewahi kuichezea TP Mazembe ya DR Congo alijiunga na Genk mwaka 2015 baada ya mkataba wake kumalizika ambaye wakati wowote huenda akatimkia England.
Akizungumza katika Kipindi cha Spoti Hausi kupitia Global TV Online, baba mzazi wa Samatta, Mzee Ally Samata alisema tayari klabu tatu kutoka England na nyingine za Hispania na Ufaransa zinamtaka.
Mzee Samata alisema, usajili wake huo hivi sasa upo chini ya wakala wake ambaye yupo kwenye mazungumzo na klabu hizo ambazo majina yake ameyaficha.
“Ninataka kumuona akicheza soka England, ninaamini atafanikiwa kwani tayari malengo hayo naona yameanza kutimia baada ya klabu tatu kutoka England kuvutiwa naye.
“Nimemwambia akubali kujiunga na timu hizo bila kujali nafasi zake katika ligi kuu kwani nina imani atazitumia kama njia ya kufika mbali zaidi.
“Ninaamini mwanangu atafanikiwa na ninataka kumuona akiichezea timu yangu ninayoipenda mimi na yeye mwenyewe ambayo ni Manchester United.
“Lakini akikosa kuichezea Man United, basi aichezee timu yoyote ya England ikiwemo Arsenal licha ya kutoipenda timu hiyo kwani ligi ya nchini huko ndiyo inapendwa zaidi duniani,” alisema Mzee Samata.