Ummy Mwalimu 'Alichofanya Makonda ni Sahihi, Zoezi la Kuwaita Wanawake lipo Kisheria"

Leo asubuhi, kupitia Kituo cha Runinga cha Clouds katika kipindi cha Clouds 360, nilimtazama na kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumzia mambo kadhaa yanayoihusu Wizara yake. Amezungumzia mambo mengi yakiwemo yatakayozungumzwa kwenye Bajeti ya Wizara yake itakayowasilishwa tarehe 19 mwezi huu.

Katika maelezo yake, aligusia zoezi linaloendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuwasikiliza wanawake waliotelekezwa na waume zao wakiwa na watoto. Kimsingi, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa zoezi hilo lipo ndani ya sheria, yaani lipo kisheria. Hii ni kwasababu, wanaowasikiliza wanawake hao ni Maafisa wa Ustawi wa Jamii ambao wana mamlaka ya kufanya hivyo.

Waziri Ummy Mwalimu ameongeza kuwa alichofanya Mkuu wa Mkoa Makonda ni kuwatia shime na ujasiri wanawake hao kwenda Ofisini kwake kusikilizwa badala ya wanawake hao kwenda kwenye Ofisi za Ustawi wa Jamii. Akasema kwa kusisitiza kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii ndiyo wanaowasikiliza wanawake hao na ikibidi wanaume watakaotajwa nao wataitwa na kusikilizwa. Kama hakutakuwa na maridhiano, mambo hayo yatapelekwa mahakamani.

Waziri Ummy Mwalimu akasema pia kuwa anaungana na Naibu Waziri wake Dr. Faustine Ndugulile kukemea kuvunja faragha za watoto katika kusanyiko hilo. Akasema kuwa ameongea na Paul Makonda na kuahidi kutatua tatizo la faragha linalojitokeza hata mitandaoni kuwahusu watoto. Amewaasa wanawake na wanajamii kwa ujumla kutowaanika watoto katika mitandao kwakuwa kwa kufanya hivyo ni kuingilia faragha zao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad