Viongozi wawili wa Baraza la la Wazee Taifa la CHADEMA, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro usiku wa kuamkia leo Aprili 17, 2018 ambapo mpaka sasa haijafahamika kusudio la kukamatwa kwao.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema wakati alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hizi na kuwataja viongozi hao waliokamatwa kuwa ni dereva Proaches Urassa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Jimbo la Morogoro Kusini Mzee Daniel Banzi.
"Jambo la kusikitisha ni kuwa jana usiku Polisi walivamia walikokuwa wamelala Viongozi na kuwakamata baadhi yao ambao walikuwa kwenye ziara ya kukutana na wazee kwenye vikao vya ndani. Hakuna maelezo ya maana yanayotolewa zaidi ya Polisi kusema ni ukaguzi wa kawaida, ila ukweli ni kwamba kila wanapoonekana viongozi wa CHADEMA Polisi wanawakamata", amesema Mrema.
Pamoja na hayo, Mrema ameendelea kwa kusema "mpaka sasa tumewatuma Mawakili wetu mkoani Morogoro ili waweze kujua viongozi hao walikamatwa kutokana na tatizo gani. Tunalaani kwa nguvu zote udhalilishaji huu unaofanywa dhidi ya viongozi na wanachama wetu".