WAMILIKI wa nyumba zinazosaidia waathirika kujinusuru na dawa za kulevya nchini maarufu kama Soba house wamejibu tuhuma za kuwachoma vijana sindano pindi wapatapo nafuu.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jiji Dar es Salaam Katibu wa Umoja wa Soba house nchini, Pili Missanah ambaye ni mmoja wa wamiliki wa vituo hivyo ameeleza kuwa, April 25 mwaka huu katika mjadala wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baadhi ya wabunge walieleza kuhusu tabia chafu za baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo kuwachoma sindano za dawa za kulevya baadhi ya waathirika pindi wanapokaribia kupona ili wazazi au walezi waendelee kuchangia fedha kwenye nyumba hizo.
Pili ameeleza kuwa lengo la nyumba hizo sio baya bali ni kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya na zinaendeshwa kwa kufuata sheria ambayo Serikali iliweka kupitia Mamlaka ya kudhibiti kupambana na dawa za kulevya na kuweka mwongozo wa kuziendesha nyumba hizo ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu.
Aidha, Pili amekanusha vikali tuhuma hizo na kueleza kuwa wanawaomba wabunge waliotoa tuhuma hizo kutoa ushahidi na watakaobainika wachukuliwe hatua na wamiliki hao wapo tayari kutoa ushirikiano, pia wameiomba Serikali kupitia mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kufanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo ambapo ameeleza kuwa hawajapata malalamiko yoyote kutoka kwa wazazi au walezi wa waathirika hao juu ya tuhuma hizo.
Ameongeza kuwa, tuhuma hizo hazitawarudisha nyuma bali zimewapa nguvu za kuendelea kupambana na kuwasaidia waathirika hao ili waweze kurudi katika hali yao ya kawaida na kuendelea kujenga taifa.
Wamiliki wa nyumba wameeleza kuwa kuna nyumba 22 pekee Tanzania na hadi sasa zina waathirika 737 wanaopatiwa matibabu wakiwemo wanawake 21 na wanaume 726 na hadi sasa wameokoa watu zaidi ya 4,000 ambao wameachana na matumizi ya dawa za kulevya na wanaendelea na shughuli nyingine za kimaendeleo.
Umoja huo umeeleza nia yao ya dhati katika kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika suala la kupiga vita suala la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na watasimamia kauli mbiu yao ya; ” Msaidie muathirika wa dawa za kulevya apate huduma ya matibabu na usimnyanyapae” na “Tuwasikilize watoto na vijana ili kuwaepusha na dawa za kulevya.”