Ni kawaida na ni utamaduni wa sehemu nyingi duniani wanaume kuchimba kaburi na kuwaachia wanawake shughuli nyingine za jikoni wakati wa msiba.
Lakini sivyo ilivyokuwa kwa wanawake wa Mtaa wa Bwihegule wilayani Geita. Wanawake hao wa Kata ya Mtakuja walilazimika kuchimba kaburi, ikiwa ni adhabu iliyotokana na tuhuma kuwa wanahusika na vifo vya ghafla vya wanaume mtaani hapo.
Tukio hilo lililoibua hisia na maoni mchanganyiko kutoka kwa walioshuhudia lilitokea Aprili 24 baada ya mkazi wa mtaa huo, Nkangiko Vigume (57), kufariki dunia ghafla Aprili 23.
Wanaume saba wafariki
Habari kutoka mtaani hapo zinasema amri ya kutaka wanawake kuchimba kaburi na kulala matanga ilitolewa na mtemi, ambaye ni kiongozi wa mila wa jamii ya Wasukuma mtaani hapo, Kahema Nsabilando.
Alitoa amri hiyo baada ya uamuzi kufikiwa kwenye kikao cha dharura kilichojadili matukio ya vifo vya ghafla vya wanaume mtaani hapo.
Wakazi waliitisha kikao hicho kujadili vifo vya ghafla vya wanaume baada ya Vigume kufariki Aprili 23 na kufanya idadi ya waliokufa kufikia saba.
“Hili ni tukio la saba wanaume wanafariki ghafla hapa mtaani kwa kuumwa kichwa. Vikao vya wananzengo vimeshafanyika na kuwaonya akina mama kuacha mambo haya (ya kuhusika na mauaji ya kishirikina ya wanaume), lakini wamerudia tena,” alisema Nsabilando.
“Tumechoshwa na lazima waadhibiwe kwa kuachwa walale matanga na kuchimba kaburi wenyewe kwa mujibu wa mila na desturi.”
Kifo na matukio ya ajabu
Akisimulia yaliyojiri kabla ya kikao kilichotoa uamuzi, Nsabilando alisema baada ya Vigume kufariki dunia, utaratibu wa kuandaa mwili kwa ajili ya mazishi ulifanyika lakini yalitokea matukio aliyodai ni ya ajabu yakiashiria kifo chake hakikuwa cha kawaida.
“Wazee tuliuandaa mwili wa marehemu na kuulaza kitandani mikono ikiwa imenyooshwa, lakini baada ya muda mfupi tuliona mikono imewekwa kifuani,” alidai.
Kiongozi huyo alidai kilichowashtua zaidi hadi kufikia uamuzi wa kutoa adhabu ni mwili huo kukutwa umelala kifudifudi licha ya kuachwa kitandani ukiwa chali.
Kuhusu vifo tata mtani hapo, Mbares Mabula ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maafa, alisema ndani ya miaka miwili kumekuwa na vifo vyenye utata vya wanaume vinavyosadikiwa kusababishwa na wanawake wanaotuhumiwa kutaka kutaka kurithi mali.
Alidai baadhi ya waliokufa na kuzikwa, wanaonekana mitaani katika mazingira yanayotatanisha, hivyo kuibua hofu ya ushirikina.
Licha ya mwandishi wa Mwananchi kuwashuhudia polisi wanne katika eneo la tukio, wawili kati yao wakiwa na silaha, kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jana kuwa ofisi yake haina taarifa hizo.
Lakini mkuu wa wilaya, Herman Kapufi alisema uchunguzi wa awali umebaini limesababishwa na imani potofu za kimila na kuahidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
“Hivi ni vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake. Serikali haiwezi kuvivumilia, tutafanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya walioamuru wanawake kuchimba kaburi ili kuvikomesha,” alisema Kapufi.
Kapufi alisema imani za kishirikiana huchochea mauaji ya watu kwa kukatwa kwa mapanga katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wanawake walonga
Baadhi ya wanawake waliofanya adhabu hiyo hawakukubaliana na uamuzi huo.
“Hatukubaliani na uamuzi, lakini hatuna la kufanya kutokana na mabavu ya wanaume ambao baadhi hutushurutisha kwa fimbo kuchimba kaburi,” alisema Specaoza Salum, mmoja wa wanawake walioshiriki kuchimba kaburi.
Mwanamke mwingine, Kabula Shija alisema pamoja na kulala matanga na kukamilisha uchimbaji kaburi kabla ya saa 7:00 mchana siku hiyo ya Aprili 24, wanaume hao pia waliwaagiza kuhakikisha wanapika na kuwapa chakula kabla ya muda huo.
Mwanamke mwingine, Suzan Mayala alisema adhabu hiyo haikujali hali zao kiafya wala majukumu ya kifamilia na kijamii kwa sababu ilihusisha wanawake wote wakiwemo wenye watoto wachanga.
Familia haikuweza kuzuia
Hata kama isingekubaliana na adhabu hiyo, familia ya wafiwa haikuwa na uwezo wa kuzuia utekelezaji wake.
Thomas Nzobano, kiongozi wa ukoo wa marehemu Vigume, alisema hawakuwa na uwezo wa kuingilia kati uamuzi wa wananzengo kwa sababu kiutaratibu hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya matanga na mazishi.
“Familia tunatakiwa kusubiri uamuzi na kufuata maagizo ya wananzengo kuhusu masuala yote ya mazishi. Hatujihusishi na kuchimba kaburi kwa kuwa hiyo ni kazi ya wanajamii,” alisema Nzobano.
Mwanafamilia mwingine, Ndakirwa Mkangiko ambaye ni mmoja wa watoto 12 wa Vigume, alisema familia imeshtushwa na kifo cha ghafla cha baba yao aliyeugua kichwa kwa muda mfupi.
Hasira zilizidi nguvu uongozi
Mwenyekiti wa Mtaa ya Bwihegule, Andrea Barnaba alisema hamaki na hasira ya wananchi kuhusu matukio ya vifo na madai ya mwili wa marehemu kugeuzwa ulipolazwa, ziliuzidi nguvu uongozi wa Serikali ya eneo hilo na kulazimika kuwaacha wananchi kuendelea na walichoamua.
“Hakuna mtu wala kiongozi yeyote aliyekuwa akisikilizwa na wananchi zaidi ya viongozi wa kimila wakiongozwa na mtemi. Kama viongozi tuliona ni busara kutotumia mabavu ili kuepuka madhara zaidi kutokana na hamaki waliyokuwa nayo wananchi,” alisema Barnaba.