Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya siasa wajitahidi kuwa makini na namna wanavyoendesha vyama vyao kwa sababu wananchi wanaowaongoza ni wa vyama vyote.
Majaliwa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa katika ukumbi wa mikutano wa Waziri Mkuu ulioko Mlimwa jijini Dodoma.
"Viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa wajitahidi kuwa makini na namna ambavyo wanaendesha siasa katika vyama vyao, wananchi wanaowaongoza ni wa vyama vyote hivyo tupeleke ujumbe ambao utawaongoza kujileta maendeleo,” Majaliwa.
Aidha Kiongozi huyo amewataka pia viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa waendelee kushikamana ili waweze kulifikisha Taifa mahali ambapo Watanzania wanapatarajia ikiwa ni pamoja na kupunguza umaskini.
Waziri Mkuu amesema kuwa mazungumzo yaliyofanyika leo baina ya Serikali na viongozi hao yameonesha nia ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano na kwamba wana wajibu wa kuendeleza historia nzuri kwani siasa ni moja ya nyenzo zinazochochea maendeleo.
Akijibu ombi la viongozi hao kuhusu changamoto ya upatikanaji wa fedha za kuendesha shughuli za baraza hilo ikiwemo mikutano, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maombi hayo ili waweze kutimiza majukumu yao kama ilivyokusudiwa.