Serikali ya Marekani imeweka kipingamizi juu ya muswada ulioletwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) Jumamosi ukitaka uchunguzi ufanyike juu ya Israeli kutumia risasi za moto dhidi ya Wapalestina walioshiriki katika maandamano katika Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa maelezo ya mwanadiplomasia wa Baraza hilo ambaye alilifahamisha shirika la habari la Ufaransa.
Vyombo vya usalama vya Palestina vimesema kwamba sio chini ya watu 15 waliuwawa Ijumaa na majeshi ya Israeli na zaidi ya watu 750 walitupiwa risasi za moto.
Wapalestina walizika maiti za watu wao Jumamosi, huku waombolezaji wakitangaza kulipiza kisasi.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamini Netanyahu aliyapongeza majeshi ya Israeli ambayo yalitupa risasi dhidi ya Wapalestina.
“Hongereni askari wetu,” waziri mkuu alisema katika tamko la serikali. “Israel inachukua hatua thabiti na kwa azma ya kulinda uhuru wake na usalama wa wananchi wake.”
Wapalestina walikuwa katika siku ya maombolezo ya kitaifa Jumamosi.
Shirika la habari la Associated Press (AP) limeripoti Jumamosi kuwa mmoja wa waandishi wake walishuhudia Wapalestina wawili, katika matukio mawili tofauti, ambao walikuwa wakitembea karibu na mpaka wa eneo lenye uzio la Ukanda wa Gaza linalotenganisha Israeli kutoka kwa Wapalestina. Wanajeshi wa Israeli waliwatupia risasi na kuwapata Wapalestina hao miguuni.
Katika tukio jingine, kijana wa miaka 16 ameiambia AP yeye alitupa mawe kuelekea katika mpaka huo siku ya Ijumaa na kutupiwa risasi zilizolenga miguu yote miwili. Kijana huyo alikuwa hospitali akitibiwa wakati mguu mmoja umefungwa bendeji na mwengine umetiwa vyuma, wakala wa habari wameripoti.