Waziri Mwigulu Awapa Makali Jeshi la Polisi

Waziri Mwigulu Awapa Makali Jeshi la Polisi
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amelitaka Jeshi la Polisi kuwa wakali kwa watu wanaofanya mzaha pindi wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ili kuweza kuokoa maisha ya watanzania yanayopotea kila kukicha kwenye ajali.


Waziri Mwigulu ametoa kauli hiyo leo katika Mkutano wa 11 wa kikao cha Bunge cha kwanza kinachoendelea kufanyika katika mkoa wa Dodoma wakati alipokuwa anajibu swali ya nyongeza la Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyetaka kusikia tamko la serikali kuhusiana na faini zinazotozwa na askari wa barabarani pindi wanapowakamata madereva wa magari badala ya kuwapa elimu elekezi.

"Sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kutoza faini au kukusanya faini sio kipaumbele chetu ila kipaumbele chetu ni maisha ya watanzania. Tunapobaini kuwepo uzembe mwingi barabarani ndipo tunapoamua kutoza faini kwa hiyo kama watanzania watazingatia na kuwa waangalifu kwamba wamebeba dhamana kubwa ya maisha ya wenzao katika vyombo vyao moto hili suala la faini litakuwa limeisha", amesema Waziri Mwigulu.

Pamoja na hayo, Waziri Mwigulu ameendelea kwa kusema "nitoe rai kwa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa wakali pindi watu wanapofanya mzaha, huku wakiwa wamebeba abiria ili kuokoa maisha yanayotokana na ajali nyingi zinazotokea barabarani, na jambo hili ninalo lisemea ni kwa vyombo vya moto vyote kuanzia magari ya abiria na binafsi pamoja na bodaboda. Nalisisitiza hili kwasababu tumeshuhudia vifo vikiwa vimetokea pindi tunapoenda katika eneo la tukio unakuta gari limekwisha andikiwa faini kutokana na kutembea mwendokasi".

Kwa upande mwingine, Waziri Mwigulu amesema ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 43 hadi kufikia Disemba 2017 ambapo katika kipindi cha mwaka 2016 jumla ya ajali 9,856 zilizosababisha vifo 3,256 na majeruhi 2,128 na mwaka 2017 ajali 5,310 ambazo zilisababisha vifo 2,533 na majeruhi 5,355 wakati kipindi cha Januari hadi Februari mwaka 2018 zimetokea ajali 769 zilizosababisha vifo 334 na majeruhi 698 ambapo katika kipindi hicho wahanga 1583 wakilipwa fidia takribani Bilioni  7 kutoka makampuni mbalimbali ya bima.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad