Yanga : Ushindi Upo Pale Pale

 Yanga : Ushindi upo pale pale
Yanga, wanawakaribisha Welayta Dicha FC kutoka Ethiopia katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwakosa nyota wake muhimu wa kikosi cha kwanza.

 Awali Yanga ilishuka uwanjani kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika bila washambuliaji wake tegemeo Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao ni majeruhi na leo inawakosa Kelvin Yondani, Pappy Tshishimbi, Said Makapu na Obrey Chirwa kutokana na kuwa na kadi za njano.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi na beki wa zamani wa timu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya Michezo ya SportPesa, Shadrack Nsajigwa, alisema jana kuwa ushindi mnono ndiyo utawaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo na si jambo lingine.

Nsajigwa alisema benchi la ufundi la timu hiyo limewaandaa wachezaji waliopo kuhakikisha wanapambana na kupata matokeo mazuri katika mchezo huo na kukubaliana na changamoto zinazowakabili.

"Msimu huu kwetu hauko vizuri, kwanza tulikuwa tunakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi, na sasa kadi za njano zinatugharimu, ila tulishajiandaa na hali hii, kabla ya kujua kama tungetolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunataka kupata ushindi, ni wazi kama tutatumia vyema uwanja wetu wa nyumbani tutakuwa tumejiweka mahali salama, ukitumia vizuri uwanja wa nyumbani unakuwa umejirahisishia safari yako," alisema Nsajigwa.

Yanga ambayo ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walihamia kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho baada ya Township Rollers ya Botswana kuwaondoka katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1.

Kikosi hicho cha Mzambia, George Lwandamina, leo kitashuka uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la FA na Singida United kwa kufungwa penalti 4-2 baada ya kutoka sare ya 1-1.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad