YANGA ni kama tayari imeshafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya bechi la ufundi la timu hiyo, kuiboresha safu ya ushambuliaji kwa kuwaongezea mbinu mbadala za ushindi katika mechi dhidi ya Wolayta Dicha ya nchini Ethiopia.
Yanga jana alfajiri ilisafiri kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumatano saa kumi kamili jioni kwa saa za Tanzania.
Katika msafara huo, wachezaji wote wamesafiri huku akikosekana kipa, Ramadhani Kabwili, Maka Edward, Said Mussa walio kwenye kikosi cha vijana wa timu ya taifa ya U20 na Ibrahim Ajibu mwenye majeraha.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema tayari wamefanyia marekebisho kwenye safu ya ushambuliaji ambayo ilisababisha washindwe kupata mabao mengi katika mchezo uliopita jijini Dar es Salaam.
Nsajigwa alisema, safu hiyo ya ushambuliaji tayari wameiimarisha ili kuhakikisha wanaitumia vema kila nafasi watakayokuwa wanaipata katika mchezo huo wa marudiano baada ya kuona udhaifu wa mabeki wa Dicha.
“Tulicheza na Dicha katika mechi iliyopita ya hapa nyumbani tukiwa hatuwajui vizuri, lakini katika mchezo huu wa marudiano, tutaingia uwanjani tukiwa tunajua udhaifu wao wakiwemo wachezaji hatari.
“Katika mechi iliyopita, wachezaji wetu wakiwemo washambuliaji, walicheza bila ya kufuata maelekezo yetu na hasa katika kipindi cha kwanza kwani tuliwaambia wacheze mipira mirefu kutokana na mabeki wa Dicha kutokuwa na kasi, lakini tukashukuru kipindi cha pili walibadilika na kucheza kwa maelekezo licha ya kushindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga mabao.
“Hivyo, baada ya kuwajua vizuri Dicha tumewaambia viungo wetu akiwemo Tshishimbi (Kabamba), Buswita (Pius) na Daudi (Raphael) kuwapigia pasi ndefu washambuliaji wetu ili wakimbizane na mabeki wa Dicha ambao tumewaona ni dhaifu kwani hawana kasi,” alisema Nsajigwa.