Abdul Nondo Amkataa Hakimu wa Kesi yake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa imeshindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wawili kati ya watano wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP) Abdul Nondo.


Hayo yamekuja baada mshitakiwa kuiandikia barua Mahakama hiyo akimtaka Hakimu John Mpitanjia anayesikiliza kesi yake ajitoa kwasababu ya kupoteza imani naye.

Katika barua yake Nondo ametaja sababu mbalimbali ikiwemo ya madai ya Hakimu huyo kukutana na mmoja wa mashahidi na kuwahoji kama wanaendelea kuwasiliana na Nondo.

Sababu ya pili, Nondo amedai kila kesi yake inapopelekwa Mahakamani RCO wa Iringa amekuwa akionekana kukutana na Hakimu Mpitanjia kabla na baada ya kesi hiyo huku sababu ya tatu ya mshitakiwa huyo akimkataa Hakimu Mpitanjia ikiwa ni mahusiano na mawasiliano mazuri na upande wa Jamhuri akiwa hana mahusiano mazuri na upande wa mshitakiwa

Abdul Nondo anashitakiwa kwa makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kuwa yupo hatarini akiwa katika eneo la Ubungo na kuzisambaza kwenye mtandao wa Whatsapp na kosa la pili limetajwa kuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga wakati alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha polisi mjini humo kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad