ACT Wazalendo Yataka Wanafunzi Waruhusiwe Kufanya Siasa Vyuoni

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuwaruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu wafanye siasa vyuoni kwa taratibu zilizowekwa kwa sababu vyuo ni kitovu cha mabadiliko ya jamii.

Wito huo umetolewa jana Mei 13 na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu ambaye anapinga kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa alipotembelea Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sua) kuwataka wanafunzi wasifanye siasa vyuoni.

Shaibu alisema historia inaonyesha kwamba viongozi wengi wa taifa hili walishawahi kuwa viongozi wa serikali za wanafunzi walipokuwa vyuoni. Amesisitiza kwamba maisha ya siasa wakiwa vyuoni ndiyo yaliwapa ujasiri wa kuingia kwenye ulingo wa siasa.

"Kupiga marufuku siasa vyuoni ni kujenga taifa la vijana waoga, wasiokuwa na uwezo wa kuhoji. Vijana msiache kuhoji mambo ya msingi kwa jamii zenu, hiyo ndiyo maana ya usomi," alisema Shaibu.

Katibu huyo alitoa mifano ya baadhi ya viongozi waliokuwa viongozi vyuoni kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Joseph Warioba ambaye amesema mwaka 1965 alikuwa mwenyekiti wa jumuiya ya wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini.

Alimtaja pia Spika wa zamani, Samuel Sitta ambaye pamoja na wenziwe walifukuzwa chuo mwaka 1966 kwa kufanya mgomo kupinga matabaka hapa nchini, ajenda ambayo Mwalimu Nyerere aliibeba kwenye Azimio la Arusha.

"Siasa za vyuo vikuu zimewekewa utarabitu wake, sasa tukianza kuwadhibiti hata vijana walio vyuoni tunatengeneza taifa la namna gani?" Alihoji Shaibu na kusisitiza kwamba serikali ina wajibu wa kuhamasisha vijana kujitosa kwenye siasa ili Taifa lipate viongozi bora siku zijazo.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad