Afya ya Ferguson Yaendelea Kuimarika Atolewa ICU

Afya ya Ferguson Yaendelea Kuimarika Atolewa ICU
Afya ya Sir Alex Ferguson inaendelea kuimarika na sasa ametoka kwenye chumba cha uangalizi maalumu alichokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Salford.

Ferguson aliwahishwa hospitali wiki iliyopita, baada ya damu kuvuja kwenye ubongo.

Awali, kocha huyo nguli wa zamani wa Manchester United, alipoteza fahamu kabla ya kufanyiwa upasuaji.

Baada ya kutolewa chumba cha wagonjwa mahututi, Ferguson mwenye miaka 76 ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari katika hospitali hiyo.

Taarifa ya mtandao wa klabu hiyo ilisema Ferguson anahitaji kupata muda mrefu wa mapumziko akiwa na familia yake.

“Familia imetoa shukurani baada ya kuungwa mkono na watu waliomtakia kila la kheri, lakini atakuwa chini ya uangalizi ili kukamilisha hatua nyingine ya uponyaji,” ilisema taarifa hiyo.

Pia kocha wa Man United, Jose Mourinho alisisitiza klabu itaendelea kumuunga mkono Ferguson na wanamtakia afya njema.

“Tuna uhusiano mzuri sana, tutaendelea kumuunga mkono, kwa sasa anahitaji mapumziko na tunaheshimu uamuzi wa familia,”alisema Mourinho.

Ferguson aliyeifundisha Man United kwa miaka 26 kabla ya kustaafu mwaka 2013 alipata ugonjwa huo Mei 5 kabla ya kuwahishwa hospitali kwa msaada wa gari la wagonjwa kabla ya kupasuliwa.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad