Baba Anayetuhumiwa Kumuua Mtoto Wake Akamatwa na Polisi

Baba Anayetuhumiwa Kumuua Mtoto Wake Akamatwa na Polisi
Mtu mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauji dhidi ya mtoto wake wilayani ukerewe.

Mnamo tarehe 23.05.2018 majira ya saa 14:00hrs mchana katika kijiji cha Hamkoko kilichopo wilaya ya Ukerewe mkoa wa Mwanza, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Buyanza Magayane miaka 39, mkulima na mkazi wa kijiji cha Hamkoko, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wa kumzaa aitwaye Baraka Buyanza, miaka 02, hii ni baada ya kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na marehemu  kujisaidia kinyesi kwenye maeneo mbalimbali ya nyumba hali iliyopelekea marehemu kupoteza maisha kisha kumzika katika shamba lake lililopo nyuma ya nyumba yake, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Awali inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa ametengana na mkewe yani mama wa marehemu kwa muda mrefu, hivyo marehemu alikua akiisha na baba yake mzazi anayetuhumiwa kusababisha kifo chake pamoja na mama yake wa kambo.

Inasemekana kuwa tarehe tajwa hapo juu mtuhumiwa alikuwa ametoka kwenye shughuli zake za kila siku ndipo aliporudi nyumbani alimkuta marehemu akiwa amejisaidia kinyesi katika sehemu tofautitofauti za nyumba yake ndipo alimchukua kisha kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kisha alimfungia ndani ya chumba peke yake.

Inadaiwa kuwa baada ya muda kupita mtuhumiwa alikwenda kumuangalia  mtoto chumbani alipokuwa amemfungia, ndipo alikuta tayari mtoto amefariki dunia.

Inasemekana kuwa baada ya kuona hali hiyo mtuhumiwa alikwenda kuchimba shimo katika shamba lake lililopo nyuma ya nyumba yake kisha alimzika mtoto, lakini majirani waliona kitendo kile kisha walitoa taarifa kituo cha polisi ambapo askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa kumakamata mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye alikiri kufanya mauaji hayo na kuwapeleka askari sehemu alipomzika marehemu.

Mwili wa marehemu tayari umefukuliwa, umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya ukerewe kwa ajili ya uchunguzi, pindi uchunguzi ukikamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Polisi wapo katika mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa walezi na wazazi akiwataka kuacha tabia ya kutoa adhabu za vipigo mara kwa mara kwa watoto pindi wanapokosea bali wawaelekeze kwa hekima na busara na kuwafundisha ili kuepusha majeruhi,ulemavu na vifo vya aina kama hii ambavyo vitapeleka mzazi kufungwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad