MUNGU ametenda! Ndiyo maneno ya kwanza kutoka kinywani kwa baba wa aliyekuwa staa wa filamu za Kibongo, Steven Charles Kanumba, Charles Kusekwa Kanumba mara baada ya kuanza mahojiano na Ijumaa Wikienda huku akieleza alivyofurahishwa na kitendo cha aliyekuwa mpenzi wa mwanaye, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kutolewa gerezani na kumpa masharti mazito mwanadada huyo.
Baba Kanumba alifunguka hayo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa njia ya simu akiwa nyumbani kwake mkoani Shinyanga, ikiwa ni siku chache baada ya mama mzazi wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa kujitokeza hadharani na kuoneshwa kutofurahishwa na kitendo cha Lulu kubadilishiwa adhabu kutoka kifungo cha miaka miwili jela hadi kifungo cha nje.
HANA TATIZO NA MTU
Tofauti na mama Kanumba ambaye alionesha kutaka Lulu abaki gerezani, baba Kanumba alisema kuwa, kutolewa kwa mrembo huyo ni mpango wa Mungu.
HUYU HAPA BABA KANUMBA
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, baba Kanumba alisema kuwa, kwanza Lulu kutolewa gerezani na kubadilishiwa kifungo cha nje ni mpango wa Mungu na alifurahishwa mno na kutoka kwake hivyo kwenye moyo wake hana kinyongo naye hata kidogo.
“Kila kitu hapa duniani hupangwa na Mungu na kila kinachotokea ni mapenzi yake, siwezi kulaumu kwa nini Lulu ametoka bali nimefurahi kwa sababu hata angefungwa miaka mia moja, Kanumba tayari alishafariki dunia, hawezi kurudi duniani.
MCHA MUNGU
“Silaumu kwa sababu mimi ni mcha Mungu hivyo Mungu ndiye amesema suala hilo lifikie tamati kwa namna hiyo, wanaopinga na kusema siyo haki, hayo ni mawazo yao maana kama ni kifo cha mwanangu kiliniuma sana, lakini sasa siwezi kumlazimisha Mungu afanye mimi binadamu ninavyotaka maana hata neno lake linatufundisha kwamba tusamehe,” alisema baba Kanumba.
AMPA MASHARTI MAZITO
Katika mazungumzo hayo na Ijumaa Wikienda, pamoja na kufurahishwa na suala la Lulu kutolewa gerezani na kupewa kifungo cha nje, baba Kanumba alimpa Lulu masharti mazito kwamba kama anataka maisha yake yaende vizuri, awe na familia nzuri kama watu wengine na amani moyoni, anatakiwa kwenda kufanya usafi kaburi la Kanumba kama ni kulia, alie na hapo atakuwa ameacha balaa na mikosi yote.
“Kwa mila za kabila letu la Kisukuma ni kwamba, Lulu alitambulika kama mke wa Kanumba maana hakuna mwanamke mwingine tunayemfahamu sisi hivyo natamani angeachiwa huru kabisa asiwe na kifungo cha nje na aende tu kufagilia kaburi la mumewe Kanumba na hapo atakuwa amemaliza na kuwa huru.
“Lulu kama anataka awe na familia, yaani aolewe, apate watoto wazuri na amani katika maisha yake, aende tu kufagilia kaburi la Kanumba na hapo atakuwa ameacha kila nuksi, balaa na mikosi hapohapo na atakuwa huru kabisa, ndiyo mila zetu zinavyosema,” alisema baba huyo.
ASIPOFANYA ITAKUWAJE?
Baba huyo aliendelea kueleza kuwa, endapo Lulu hatafuata na kufanya masharti hayo, basi atakuwa na wakati mgumu mno kwenye maisha yake kwa maana damu hiyo na mzimu wa Kanumba utakuwa ukimfuatilia na anaweza asiolewe au kupata familia, yaani watoto.
“Kinachotakiwa hapa, Lulu anatakiwa afuate tu hayo masharti ya kimila niliyompa, lakini asipofanya hivyo atajikuta akikosa amani katika maisha yake kwani kufanya hivyo kunamuepusha na kufuatiliwa na ule mzimu au damu ya Kanumba ambayo itamtesa na kujikuta akikosa furaha na amani,” alisema baba Kanumba.
MAMA LULU ANASEMAJE?
Ijumaa Wikienda lilimtafuta mama mzazi wa Lulu, Lucrecia Karugila baada ya kukutana na ugumu wa kumpata Lulu, lakini hata hivyo simu yake iliita bila kupokelewa.
MTU WA KARIBU ANENA
Mmoja wa watu wa karibu na familia ya Lulu ambaye aliomba hifadhi ya jina, alipotakiwa kuzungumzia masharti hayo ya baba Kanumba, alisema kuwa, familia imeyapokea na yanatekelezeka.“Kikubwa kwanza familia inamshukuru Mungu kwa kitendo cha kubadilishiwa adhabu ya gerezani na kumalizia kifungo chake cha nje.
“Unajua jambo lenyewe kama alivyosema baba Kanumba ni mipango ya Mungu tu. Familia haikutegemea kabisa kama Lulu anaweza kubadilishiwa adhabu.
“Unajua kama familia, baada ya hukumu ya miaka miwili kutolewa na Mahakama Kuu, Novemba, mwaka jana, licha ya kumuombea Lulu atoke, lakini kibinadamu tulikuwa tunajua ndiyo mpaka amalize miaka yake miwili gerezani ndiyo atoke,” alisema mtu huyo na kuongeza:
“Lilipokuja lile la msamaha wa Rais, nalo familia iliona tu ni kama Mungu anasikiliza maombi na kumpunguzia ile robo ya kifungo, lakini hakuna aliyekuwa anajua kwamba Lulu anaweza kutoka mapema hivi akiwa angali na miezi sita tu gerezani.”
MITANDAONI KWACHAFUKA
Mara baada ya Lulu kubadilishiwa kifungo hicho, mitandaoni kulichafuka kwa watu kumzungumzia mrembo huyo huku wengi wakionesha kufurahishwa na kitendo hicho.“Ni jambo la kheri sana. Lulu anapaswa kumshukuru Mungu kwa sababu sidhani kama alitegemea kama siku moja anaweza kutoka katika mazingira kama yale,” alichangia mdau mtandaoni.
Watu wengi kwenye mitandao ya kijamii walisema kuwa, Lulu ni binti ambaye alikuwa ana msaada mkubwa katika familia yake hususan mama yake mzazi hivyo kitendo cha yeye kurudi uraiani kinaleta faraja kubwa.
Walisema kama mzazi, kitendo cha kutomuona mwanaye kwa muda mrefu kilikuwa kinampa mawazo na hivyo sasa ni wakati wa kuanza ukurasa mpya wa maisha ya furaha.
TUJIKUMBUSHE
Mwishoni mwa mwaka 2017, Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ilimuhukumu Lulu kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake, Kanumba, lakini Mei, mwaka huu mahakama hiyo ilimbadilishia adhabu na kumpa kifungo cha nje ambapo amekuwa akifanya kazi za kijamii kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar.
MCHANGANUO ULIVYOKUWA
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Magereza, mfungwa yeyote (isipokuwa wa kunyongwa na kufungwa maisha) anapoingia tu gerezani anapata msamaha wa theluthi moja ya kifungo chake.
Hivyo Lulu alipoingia tu gerezani, alipata msamaha huo ambapo alipunguziwa theluthi hiyo na kubakiwa na miezi 16 badala ya ile 24 aliyohukumiwa mahakamani.
RAIS AMUOKOA
Baadaye, Rais Dk John Pombe Magufuli kupitia msamaha alioutoa Aprili 26, mwaka huu jijini Dodoma katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar aliwapunguzia wafungwa mbalimbali nchini robo ya vifungo vyao ambapo Lulu naye alinufaika na msamaha huo.
Hivyo kutoka kwenye miezi 16 iliyobaki, Lulu akabakiwa na miezi 12. Baadaye, Mahakama Kuu kupitia vipengele vya sheria, iliweza kumbadilishia kifungo Lulu baada ya kutumikia nusu ya kifungo chake yaani miezi 6.