Rais Nicolas Maduro ameamuru mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani aondoke nchini Venezuela baada ya kuwekewa vikwazo vingine kufuatia uchaguzi uliomrejesha madarakani Jumapili.
Maduro alitangaza hatua hiyo Jumanne kupitia televisheni ya taifa baada ya kutangazwa rasmi kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika Jumapili.
"Himaya hiyo haitutawali hapa," alisema Maduro na kuwapa saa 48 mwambata wa kisiasa Todd Robinson na naibu wake Brian Naranjo kuondoka. "Tumechoshwa na njama zenu."
Aliwashutumu wawili hao kwa kuhujumu uchaguzi wa rais wa Venezuela kwa kuwashinikiza wagombea kadhaa wa upinzani wasishiriki katika mbio hizo. Maduro alimtaja Naranjo kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA) nchini Venezuela.
Uchaguzi huo ulisusiwa na vyama vikuu vya upinzani na ulishutumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa. Vyama vya siasa viliamua kutoshiriki baada ya maofisa kuwazuia viongozi wao mashuhuri kushiriki uchaguzi.
Maduro alishinda kwa asilimia 68 ya kura lakini asilimia 52 ya wapigakura hawakujitokeza idadi ambayo ni kubwa katika historia ya nchi hiyo watu kususia uchaguzi.
Ikulu ya White House iliutaja uchaguzi huo kuwa "ulaghai", na Rais wa Marekani Donald Trump aliidhinisha amri iliyoiwekea Venezuela ukomo wa uwezo wa kuuza mali zake na hivyo kuongeza shinikizo kwa serikali ya Maduro inayokabiliwa na ukata.