Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ameitaka serikali iiondoe bungeni Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2018/19, kwa sababu imejaa kasoro zinazotakiwa kurekebishwa kabla haijapitishwa.
Amesema bajeti hiyo inatakiwa kurekebishwa kabla haijapitishwa kama ilivyo kawaida ya wabunge kupitisha bajeti zenye kasoro kama ilivyofanyika juzi katika bajeti ya Wizara ya Kilimo iliyokuwa na kasoro mbalimbali.
Bashe ameyasema hayo bungeni leo Mei 18, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2018/19 iliyowasilishwa juzi na Waziri wa Wizara hiyo, Luhaga Mpina.
Amesema hoja za baadhi ya wabunge zinazohusu maisha ya wananchi zinafia katika vikao vya vyama vya siasa.
“Naweza kuonekana mbaya kila ninapokuwa nikiikosoa serikali lakini nitaendelea kusema ukweli kwa kuwa nilianza kuwa na kadi ya CCM kabla sijawa mbunge,” amesema Bashe.
Bashe alieleza jinsi Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alivyowahi kuitwa na Kamati ya Bunge ya Uongozi baada ya kutaka kuwasilisha hoja ambayo haikuwafurahisha baadhi ya watu.