Bila TID Hakuna Msanii Bongo Angepajua Ulaya- Steve Nyerere

Msanii wa filamu nchini Steve Nyerere amedai kwamba msanii wa muziki Khalid Mohamed maarufu kama TID ndiyo msanii kutoka Tanzania ambaye alifungua milango kwa wasanii wengine wa muziki nchini kwenda kufanya matamasha nchi za Ulaya na Marekani.


Steve Nyerere amesema hayo jana Mei 12, 2018 katika kipindi cha Friday Night Live kinachorushwa na EATV kila siku ya Ijumaa saa 3:00 usiku, na kuongeza kuwa kwasasa wawili hao wamemaliza tofauti zao zilizodumu kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

“TID ni msanii wa kimataifa ambaye amefungua milango kwa wasanii wengine, bila TID hakuna msanii mwingine alikuwa anawaza kwenda Ulaya kufanya show, TID ni kitengo cha burudani ambacho kinafanya utalii wa kitaifa, TID ni mtu mwingine, ana nafasi ya kupewa dibaji, aliweza kupeperusha bendera na kushawishi vijana wengi” amesema Steve Nyerere.

Steve Nyerere aliongeza kuwa TID ni kama ndugu yake na hivyo haoni sababu ya kutomaliza tofauti zao kwakuwa wawili hao wanatoka kijiji kimoja.

February 24, 2017 katika kipindi cha 5SELEKT kinachorushwa na kituo cha EATV, msanii wa muziki TID aliahidi kufungua kesi mahakamani dhidi ya Steve Nyerere kwa sababu masanii huyo wa filamu alimtuhumu yeye kuhongwa shilingi milioni mbili na serikali ili akiri hadharani kwamba alikua anatumia madawa kulevya.


EATV

Top Post Ad

Below Post Ad