Wakati habari za simba kuonekana katika baadhi ya maeneo ya vijiji vilivyopakana na mbuga za wanyama zikiendelea kusikika, diwani wa Kimbiji wilayani Kigamboni, Bunaya Sanya amedai kuwa uwapo wa wanyama hao katika kata hiyo kunatishia usalama wa wananchi wake.
Akizungumza jana katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kigamboni, alisema simba hao ambao wapo watatu walianza kuonekana mwaka 2017 katika mitaa ya Minondo na Ngobanja.
Kikao hicho kilikuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka kata tisa za halmashauri hiyo.
“Wafugaji ndiyo waliwaona simba hawa, mwaka jana walikula mbuzi sita waliokuwa katika banda na mwaka huu wameonekana wakila nguruwe pori. Hii ni hatari tunaomba wataalamu idara ya wanyama pori washirikiane na manispaa kufanya uchunguzi ili kuwaibani,” alisema Sanya.
Alifafanua kuwa uchunguzi huo utasaidia kwa kiasi kukamatwa kwa simba hao ambao watapelekwa maeneo husika kwa ajili ya kufugwa.
Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Stephen Katemba alisema watalifuatilia suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika na kuwataka wakazi wa maeneo hayo wakiwaona watoe taarifa haraka.
Akizungumzia miradi ya maendeleo, Katemba alisema manispaa hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa kituo cha kisasa cha afya kitakachogharimu Sh500 milioni.
“Kituo hiki kinatarajiwa kukamilika mwezi huu na kitakuwa na huduma zote zikiwamo za X-ray na chumba cha kuhifadhi maiti nane kwa wakati mmoja,” alisema Katemba.
Meya wa Kigamboni, Maabadi Hoja aliwashukuru watendaji na madiwani wa manispaa hiyo kwa kufanya kazi kwa ushirikiano.