Mniache! Ndivyo alivyosema aliyewahi kutikisa na msemo wa 900 Itapendeza, Dk. Luis Shika baada ya kusikia warembo Bongo wameanza ‘kunyapianyapia’ mabilioni yake ya fedha aliyodai yamefika nchini yakitokea Urusi.
Dk. Shika ambaye alijipatia umaarufu kupitia mnada wa nyumba za Lugumi na kudai ana mabilioni ya fedha yamezuiliwa nchini Urusi, katikati ya wiki hii ameibuka na kusema sehemu ya fedha zake, takriban dola milioni 60 za Marekani (zaidi ya shilingi bilioni 135) tayari zimewasili nchini.
Katika klipu iliyosambaa mitandaoni, Dk. Shika amesikika akieleza namna fedha hizo zilivyoingia nchini pamoja na taratibu zinazoendelea za kuzihakiki na ndipo baadhi ya warembo wa Kibongo walipoanza kumtafuta.
“Jamani naombeni namba ya Dk. Shika, namtafuta kwa namna yoyote ile,” mrembo aliyejitambulisha kwa jina la Amina alisema alipopiga simu dawati la Risasi Jumamosi huku pia wengine wengi wakipiga simu chumba cha habari.
Kama hiyo haitoshi, chanzo kingine kililiambia Risasi Jumamosi kuwa mbali na warembo ambao ni watu wa kawaida, wapo baadhi ya mastaa wa kike ambao wanahaha kuitafuta namba ya Dk. Shika baada ya kusikia fedha zimetua. “Yani mastaa wanahaha kweli mimi nakwambia fuatilieni,” kilisema chanzo.
Alipoulizwa kuhusu kupata usumbufu huo kwa mabinti, Dk. Shika alisema kwanza hashobokei wanawake na bahati mbaya hapokei simu ambazo hazijui.
“Waniache. Mimi fedha zangu ni kwa ajili ya kufungua kampuni na kuwaajiri watu. Hizo simu wanaweza kuwa wanapiga lakini bahati mbaya sana sipokei simu nisiyoijua hivyo watahangaika bure,” alisema Dk. Shika.
Dk. Shika alijizolea umaarufu katika mnada wa nyumba za mfanyabishara Said Lugumi ambapo alizua gumzo baada ya kupanda dau la mnada hadi kufikia shilingi milioni 900 ambapo hata hivyo, alipoambiwa atoe hakuwa nazo hali iliyomfanya akamatwe na kuwekwa rumande polisi.
Hata hivyo, baadaye Dk. Shika aliyekuwa akisisitiza kuwa fedha zake zipo na zimezuiliwa kwa muda nchini Urusi, aliachiwa baada ya kujidhamini mwenyewe na akawa anaendelea na shughuli zake hadi katikati ya wiki hii alipoibuka upya na kusema mamilioni ya fedha zake zimewasili nchini huku akija na msemo mpya akisema ‘mtaelewa"