Ewura Yatangaza Kushusha Bei ya Petrol, Dizeli na Mafuta ya Taa

Ewura Yatangaza Kushusha Bei ya Petrol, Dizeli na Mafuta ya Taa
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa asilimia 0.9 hadi asilimia 3.8 kuanzia kesho, Mei 2.

Taarifa iliyotolewa leo Mei Mosi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzingagwa Mchany amesema bei hiyo ni kwa upande wa  Tanzania bara.

Hata hivyo, punguzo hilo ni kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia katika bandari ya Dar es Salaam huku watumiaji wa bandari ya Tanga bei ikiongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ikilinganishwa na tangazo la bei ya mafuta la Aprili 4, bei ya petroli imepungua kwa Sh88 kwa lita (asilimia 3.8) na dizeli Sh61 kwa lita (asilimia 2.75) huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Sh2 kwa lita sawa na asilimia 0.09.

Kadhalika bei ya wanunuzi wa jumla wa bidhaa za petroli nayo imepungua kwa Sh100.91 kwa lita (asilimia 4.58), dizeli Sh73.71 kwa lita (asilimia 3.52) na mafuta ya taa ni Sh10.49 kwa lita sawa na asilimia 0.51.

Mafuta yanayopita bandari ya Tanga bei yake kwa wanunuzi wa rejareja imeongezeka kwa asilimia 0.14 kwa petroli na asilimia 0.71kwa dizeli lakini wauzaji wa jumla bei imepungua kwa asilimia 0.46 (Sh9.8 kwa lita) kwa petroli na asilimia 0.1 (Sh1.9 kwa lita) kwa dizeli.

“Hakuna uingizaji mpya wa mafuta uliofanyika nchini kupitia bandari ya Tanga lakini kutokana na mabadiliko ya bei ya Ewura lakini kuna mabadiliko ya bidhaa hizo tofauti na ilivyotangazwa Aprili 4. Bei ya petrol itaongezeka kwa sh3 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh15 kwa lita,” imeeleza taarifa hiyo.

Kutokana na kupungua kwa mafuta ya taa katika bandari, watumiaji wa mafuta ya taa wa mikoa ya nyanda za juu ambao hutumia bandari hiyo, wameshauriwa kuchukua bidhaa hiyo katika bandari ya Dar es Salaam kwa bei elekezi.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad