UTAMU wa ubuyu hauchagui mtoto wala mtu mzima, wote ni twende tu! Mwigizaji wa sinema za Kibongo ambaye ni mzazi mwenza wa Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) anayetumikia kifungo cha miezi mitano jela, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Faiza Ally amejikuta akimwaga machozi laivu!
Kwa mujibu wa msambaza ubuyu wetu, hivi karibuni Faiza alinasa ujauzito mwingine wa mtoto wa tatu huku mtoto wake wa pili akiwa na umri wa miezi nane tu kisha ukachoropoka. Chanzo hicho kilitiririka kuwa, Faiza alianza kuumwa bila kujua anaumwa nini baada ya kuwa anatumia dawa akiamini ni za kuzuia ujauzito, kumbe zilikuwa ni za kuharibu mimba.
Ilisemekana kwamba, Faiza alifikia hatua ya kutumia dawa hizo akiamini hatapata mimba kwa kuwa baba wa mtoto wake wa pili alikuwa amekuja Bongo kwa kuwa ni raia wa Marekani. Kiliendelea kutiririka kuwa, Faiza alikuwa haelewi, lakini kila alipotumia dawa hizo alipata maumivu makali na kuanza kuona mabadiliko makubwa kwenye mwili wake, hasa wakati wa hedhi.
Ilisemekana kwamba, kufuatia hali hiyo, ilimlazimu Faiza kwenda kuonana na daktari ili kujua ni kitu gani kinamsumbua. “Alipoamua kwenda hospitalini alikuwa hajui tatizo ni nini kwenye mwili wake. Kila alipokuwa akitumia dawa hizo zilimfanya ajisikie vibaya mno.
“Pale kwenye Hospitali ya AAR ndiyo waligundua kuwa alikuwa na ujauzito ila ulishaanza kutoka na kubaki masalia ambayo ilibidi asafishwe,” alitonya mtoa ubuyu wetu. Mpashaji huyo alizidi kuweka wazi kuwa, baada ya kugundulika kwamba alikuwa na ujauzito, lakini ukawa umeharibika kutokana na dawa hizo, madaktari waliamua kumsafisha ili kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida.
Baada ya gazeti hili kupata ubuyu huo lilimtafuta Faiza ili kufafanua zaidi kuhusu ishu hiyo ambapo mambo yalikuwa hivi;
Ijumaa Wikienda: Pole sana Faiza na kuumwa?
Faiza: Asante.
Ijumaa Wikienda: Tumepata habari kuwa ulikuwa mjamzito, hilo limekaaje?
Faiza: Ndiyo…ni kweli nilikuwa na ujauzito.
Ijumaa Wikienda: Sasa ilikuwaje wakati una mtoto mdogo?
Faiza: Ilitokea tu bahati mbaya!
Ijumaa Wikienda: Eeh!
Faiza: Unajua mimi sikai na baba mtoto wangu hivyo mara nyingi tunatumia dawa ya kuzuia mimba, lakini tuliyokuwa tukitumia ilikuwa siyo ya kuzuia ni ya kuharibu mimba hivyo ujauzito huo ulipoingia kwa bahati mbaya na kutumia dawa hizo, ukatoka. Lakini haukutoka vizuri, ndiyo nikawa ninajisikia kuumwa hadi nilipochukua uamuzi wa kwenda hospitalini.
Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo kama isingekuwa ni hiyo dawa kuharibu na mimba imeingia bahati mbaya ungezaa?
Faiza: Ndiyo maana Mungu angekuwa amepanga. Mimi siwezi kutoa ujauzito hata siku moja.
Ijumaa Wikienda: Lakini si ulisema watoto wawili wanatosha?
Faiza: Ndiyo ilikuwa hivyo, lakini mimba imeingia bahati mbaya, nisingeweza kufanya lolote zaidi ya kusubiri kulea tu kwa mara nyingine.
Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo hospitalini wakafanyaje?
Faiza: Walinisafisha na sasa ninaendelea vizuri.
Ijumaa Wikienda: Polesana Faiza.
Faiza: Asante