Azizi Kombe, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ziba, alimtaja aliyeuawa ni Mwajuma Masanja (37), mkazi wa Kijiji cha Iduguta wilayani Nzega na Shija Maneno (35), mkazi wa Kitongoji cha Ipuli Kijiji cha Igumila Kata ya Ziba ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufani Nkinga na hali yake ni mbaya.
Mtendaji huyo alifafanua watu hao walikuwa ni mtu na mpenzi wake ambao walikuwa wakinywa pombe za kienyeji kwenye klabu iliyopo Kata ya Ziba na kuongeza kuwa baada ya kufika saa 3 usiku waliamua kuondoka kurudi nyumbani.
Hata hivyo, Kombe alibainisha wakati wakiwa njiani kurejea nyumbani walishambuliwa na fisi eneo la vichaka ambapo alimng’ata Mwajuma sehemu za makalio na tumboni, hali iliyomlazimu Shija amsaidie huku akipiga kelele za kuomba msaada.
Mtendaji huyo alisema wakati mwanaume huyo akitoa msaada kwa mpenzi wake, ndipo fisi alimng’ata usoni na ndipo aliposhindwa kutoa msaada na fisi huyo aliendelea kumshambulia mwanamke huyo hadi alipopoteza maisha papo hapo.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, muda mfupi wananchi walifika eneo hilo wakiwa na baadhi ya askari wa kituo kidogo cha polisi Ziba kisha kufanikiwa kumuua fisi huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Willibrod Mutafungwa, alithibitisha kuuawa kwa mwanamke huyo kwa kushambuliwa na fisi na kwamba fisi huyo aliuawa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, majeruhi alikimbizwa Hospitali ya Rufani ya Nkinga ambako alilazwa na kutoa wito kwa wananchi mkoani Tabora kuwa makini na wanyama hatari kwa kutotembea usiku kwenye maeneo hatarishi kwa ajili ya usalama wao.