Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Mabingwa wa Ligi Kuu (VPL) Simba SC, Haji Manara amefunguka na kuivaa klabu ya Azam FC kuwa hawakuweza kutambua mapema thamani ya nyota wao wanne wa msimu uliopita ambao ndio wameipatia ubingwa Simba msimu wa mwaka 2017/18.
Manara ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa kijamii mchana wa leo Mei 21, 2018 mara baada ya klabu yake mwishoni mwa wiki iliyoisha kukabidhiwa kikombe cha ushindi wa ligi kuu Tanzania Bara licha ya kufungwa na Kagera Sugar bao 1-0 mchezo uliochezwa katika dimba la Taifa Jijini Dar es Salaam.
"Nilimwambia aliyekuwa CEO wa Azam FC, Abdul Mohamed kuwa Aisha Manula, John Bocco, Erasto Nyoni pamoja na Shomari Kapombe mnawaona hawafai leo lakini ndio watakaotupa ubingwa msimu huu", amesema Manara.
Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "ni nani anaebisha mchango wa hawa wanaume wanne kwenye ubingwa wetu? kwa ujumla wamefunga goli 18, wame-assist 19 huku Manula akiwa na 'clean sheets' 20 pamoja na kazi kubwa ya wachezaji wote wa Simba. Huwa najiuliza bila hawa sijui ingekuwaje?".
Ubingwa wa ligi kuu msimu huu ni wa kwanza kwa Simba tangu Haji Manara awe msemaji wa timu hiyo na kumfanya aweze kutimiza malengo yake ya siku zote ya kutamani siku moja wamechukua ubingwa kabla ya yeye kuihama klabu hiyo endapo itatokea kufanya hivyo.