Huduma ya kwanza ni matibabu ya awali anayopata mgonjwa mara tu au muda mfupi baada ya kugongwa na nyoka kabla hajafikishwa kwenye kituo cha afya. Inaweza kufanywa na muathirika mwenyewe au mtu yeyote mwenye ujuzi wa kutoa huduma ya kwanza aliyepo karibu.
Malengo ya huduma ya kwanza
Kujaribu kuzuia kusambaa kwa sumu
Kulinda uhai na kuzuia madhara kabla mgonjwa hajapata matibabu
Kudhibiti dalili hatarishi za sumu
Kuandaa usafiri wa kumpeleka mgonjwa kwenye kituo cha tiba
Muhimu zaidi, Ni kuepuka kusababisha madhara zaidi.
Hatua za Huduma ya Kwanza
1. Mtie moyo mgonjwa (mara nyingi anakuwa na hofu).
2. Mlaze mgonjwa katika hali ya utilivu, hakikisha viungo havichezi . Viungo vikicheza huchangia sumu kusambaa mwilini.
3. Epuka kugusa sehemu iliyogongwa. Unapogusa sehemu iliyogongwa unasababisha sumu kusambaa kwa urahisi, kuingiza vimelea vya bakteria na damu kuvuja.
KUMBUKA : Iwapo nyoka ameuwawa unaweza kwenda nae katika kituo cha afya.