Jaji Mkuu Awataka Viongozi na Watendaji wa Mahakama Kutenda Haki

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewataka viongozi mbalimbali wa mahakama ikiwemo Naibu Wasajili, Mahakimu, Watendaji, Wakuu wa Idara na Vitengo kutenda haki kwa watumishi walio chini yao.

Jaji Mkuu ameyasema hayo leo Mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa baraza la wafanyakazi wa mahakama Tanzania.

“Sisi kama wasimamizi wakuu wa haki nchini tunawajibu mkuu wa kutenda haki kwa watumishi kwa vitendo, ni ukweli usiopingika kwamba kimbilio la mtumishi yeyote aliyefikwa na matatizo ni kwa kongozi wake katika sehemu yake ya kazi, hivyo basi kila kiongozi anapaswa kufungua milango kwa watumishi waliopo chini yake” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa, ubora wa viongozi unapimwa kwa namna wanavyosaidia wafanyakazi walio chini yao, hivyo kuwataka viongozi hao kutokufunga milango yao kwa watumishi wanaowaongoza.

Aidha, Jaji Mkuu amebainisha baadhi ya mafanikio ya kushirikisha wafanyakazi kwa lengo la kukuza motisha na kuleta ufanisi katika maeneo ya kazi na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Umihimu wa kushirikisha wafanyakazi usilenge tu katika mabaraza haya ya wafanyakazi bali uwe endelevu ili wafanyakazi wajione ni sehemu ya mabadiliko yanayoonekana” amebainisha Jaji Mkuu.

Hata hivyo Jaji Mkuu ametoa rai kwa viongozi hao kufanya kazi kwa upendo, kutoa taarifa mbalimbali kwa wafanyakazi hali itakayopelekea kupunguza baadhi ya migogoro katika maeneo ya kazi.

Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Mahakama Tanzania umewashirikisha wajumbe kutoka kanda zote na menejimenti ya Mahakama Tanzania.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad