Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Jijini Dar es Salaam na kusema kwa mujibu wa Sheria ya Magereza Sura ya 58 kifungu Na. 49 (1),(2)(3) mfungwa yeyote (isipokuwa mfungwa wa kunyongwa na wa maisha) mara baada ya kupokelewa gerezani hupata msamaha wa theluthi ya kifungo chake 1/3 ambapo Lulu alipata msamaha huo na alitakiwa kuachiwa huru Marchi 12, 2019.
Aidha, taarifa hiyo iliendelea kufafanua baadhi ya mambo kuwa katika kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Magufuli kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa msamaha wa robo ya adhabu kwa wafungwa wote waliokuwa na sifa za kunufaika na msamaha huo.
"Kufuatia msamaha huo mfungwa Na. 1086/2017 Elizabeth Michael naye alinufaika na msamaha huo na hivyo kutakiwa kutoka gerezani Novemba 12, 2018", imesema taarifa hiyo
Pamoja na hayo, taarifa hiyo imeendelea kwa kusema "kwa mujibu wa Sheria Na. 3 (2)(a) cha Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu hunufaika na utaratibu huo ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya shughuli au kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii. Mfungwa Na. 1086/2017 Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, kutokana na kukidhi vigezo vya kisheria na kuonesha tabia njema akiwa gerezani amenufaika na utaratibu huo".
Muigizaji Elizabeth Michael alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela mnamo Novemba 2017, kwa kosa la kumuua bila kukusudia muigizaji mwenzake Steven Kanumba.