Joka la Ajabu Lazua Kizaa zaa Ndani ya Daladala

DUNIA ina mambo! Joka la ajabu aina ya chatu, hivi karibuni lilizua tafrani ya aina yake ndani ya daladala na kusababisha kizaazaa huku watu kibao wakijazana eneo la tukio, Wikienda linakujuza.



Tukio hilo la kushangaza lilitokea Ijumaa kwenye daladala linalofanya safari zake kati ya Kimara na King’ongo jijini Dar.

Mashuhuda walieleza kuwa joka hilo liliibukia kwenye gari hilo aina ya Benz Saloon linalobeba abiria, hali iliyowalazimu askari wa Kituo cha Polisi cha Mbezi-Louis kufika eneo la tukio baada ya kupigiwa simu na wananchi waliokuwa na taharuki.



Waliendelea kusema kuwa daladala hilo lilikuwa maeneo ya Kimara-Moravian likiendeshwa na mafundi gereji waliokuwa wakilijaribu baada ya kulifanyia matengenezo. Mafundi hao, wakiwa wanaendesha gari hilo ndipo mmoja wao akaliona joka hilo na kumuonesha mwenzake hivyo wakalisimamisha gari hilo kisha kutoka nduki.



Wakiwa katika taharuki, wananchi walijaa eneo hilo ambapo mafundi hao waliwasiliana na mwenye gari hilo waliyemtaja kwa jina la Roshi ambaye aliwaachia daladala hiyo waitengeneze. Baada ya kumpigia simu mwenye gari hilo aliwaambia nyoka huyo ni wa jamaa ambaye alimpakia, lakini aliposhuka huenda nyoka huyo aliyemtaja kuwa ni aina ya chatu alimsahau kwenye gari hilo.



Mafundi hao walisema kuwa, Roshi aliwaeleza hivyo na kuwaahidi kuwa angemtuma mwenye nyoka wake kumfuata huku akiwaomba mafundi hao na watu wengine wasimdhuru labda kama angewaponyoka na kuingia mitaani. Baada ya kizaazaa hicho, mafundi hao walishindwa kuliendesha tena gari hilo hivyo ilibidi livutwe kwa kutumia gari lingine kwa kumhofia chatu huyo.



Kufuatia sakata hilo, Ijumaa Wikienda lilifika eneo la tukio na kuzungumza na mmoja wa mafundi hao aliyejitambulisha kwa jina la Khalid Shaban ambaye alisema kuwa, baada ya kuliona joka hilo walipatwa na mshtuko, lakini mioyo yao ilipoa baada ya mwenye gari hilo kuwaambia kwamba chatu huyo ni wa jamaa yake na kuwatoa hofu kuwa hana madhara.



“Kwa kweli tulipatwa na mshtuko mkubwa, hali iliyosababisha tuwapigie simu polisi wa Kituo cha Mbezi-Louis ambapo walifika, lakini tulivyowaambia mwenye gari amesema anamfahamu mwenye nyoka na hana madhara, waliondoka zao.



Hadi Ijumaa Wikienda linaondoka eneo la tukio, joka hilo la ajabu bado lilikuwa halijatolewa ndani ya gari hilo wala mwenyewe alikuwa hajafika kuchukua joka lake

Stori: Richard Bukos, Dar

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad