Kamati ya Bunge Kumuhoji Mugabe Jumatano

Kamati ya Bunge Kumuhoji Mugabe Jumatano
Kamati ya Bunge imepanga kumhoji Rais wa zamani Robert Mugabe Jumatano kuhusiana na upotevu wa dola za Marekani 15 bilioni katika operesheni za madini ya almasi mnano mwaka 2016.

Awali, Mugabe alitarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Madini Mei 9 siku iliyotarajiwa ya kwanza kwa kiongozi huyo mkongwe kuonekana hadharani tangu alipoondolewa Novemba 2017 lakini hakuwa amepelekewa barua ya kuitwa bungeni.

Bunge linamhitaji mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 94 kutoa maelezo juu ya tangazo lake kwamba Serikali ilikoseshwa na kampuni za madini kiasi cha dola za Marekani 15 bilioni katika mapato ya almasi.

Taarifa ya Bunge inasema Mugabe atajibu maswali Jumatano ikiwa itakuwa imethibitishwa. Hakukuwa na maelezo zaidi.

Lakini ofisa mmoja wa Bunge mwenye uelewa wa suala hilo alisema upo uwezekano mdogo kwa Mugabe kufika kwenye kamati kwa sababu ya upinzani kutoka kwa maofisa kadhaa na wanasiasa wenye ushawishi ndani ya Zanu-PF.

“Wanasema hawataki mzee wao asumbuliwe na wabunge wa upinzani. Kamwe haitatokea,” alisema huku akikataa asitajwe jina kwa vile si msemaji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Temba Mliswa alisema Bunge lilimwandikia barua Mugabe na aliipokea. Hata hivyo, hakuthibitisha ikiwa atafika kwenye mahojiano.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad