Kenya Kuzindua Setillaiti ya Kwanza ya Kihistoria Ijumaa

Kenya Kuzindua Setillaiti ya Kwanza ya Kihistoria Ijumaa
Ijumaa Kenya inatarajiwa kuweka historia kwa kuwa na setilaiti ya kwanza kuwahi kutengenezwa nchini humo itayotumwa katika sayari.

Chombo hicho cha kuzunguka sayari kilitengenezwa na wanafunzi na watafiti wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa ushirikiano na shirika la teknolojia za sayari la Japan Space Agency (JAXA).

Naibu makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Peter Mbithi amesema mafanikio hayo ni dhihirisho ya hatua zilizopigwa nchini kuhusu utafiti wa kiteknolojia ambao unaweza kuchangia katika maendeleo yatakayokuza uchumi wa kitaifa.
Setilaiti hiyo yenye ukubwa wa sentimita kumi kimchemraba itarushwa kwenye sayari kutoka kituo kilichopo Japan, lakini Wakenya kadhaa watapewa nafasi kushuhudia matukio hayo katika Chuo Kikuu cha Nairobi na yatarushwa moja kwa moja.

“Kutakuwa na tukio Japan, katika sayari na hapa chuoni  kile kitakachofanyika Japan kitashuhudiwa na baadhi ya Wakenya ambao watakuwa huko. Hapa tutakuwa na hafla katika ukumbi ambako matukio yatarushwa  moja kwa moja. Tunasubiri siku hiyo kwa hamu,” amesema Profesa Mbithi.



Wale ambao wangependa kuhudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa Chandaria uliopo chuoni hapo, watahitajika kutuma maombi kwenye tovuti ya chuo hicho na watafahamishwa kama wamebahatika kupata nafasi.



Profesa Mbithi ameongeza kuwa setilaiti hiyo itatumiwa kukusanya data kuhusu masuala mbalimbali muhimu kama mabadiliko ya hali ya anga, uhifadhi wa wanyamapori, utabiri wa hali ya hewa miongoni mwa mengine.

Ametoa wito kwa wadau wengine waungane nao ili kuimarisha zaidi utafiti kuhusu masuala ya sayari, kutia nguvu chombo hicho ili kifanikiwe kutimiza malengo yake.

Mkuu wa taasisi ya mafunzo ya uhandisi katika chuo hicho, Profesa Jackson Mbuthia amesema setilaiti hiyo yenye uzani wa kilo 14 itasafirishwa hadi kwenye sayari mwendo wa saa saba mchana Ijumaa.

“Huu ni mwanzo wa safari ambayo itawezesha Kenya kushiriki kwenye sayansi ya sayari. Ni mara yetu ya kwanza kupiga hatua hii lakini tunaamini ni muhimu katika ustawishaji wa sayansi nchini,” amesema.



Tags

Top Post Ad

Below Post Ad