Na Hamza Temba-WMU-Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemteua mshindi wa taji la Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous.
Amefanya uteuzi huo mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma baada ya mazungumzo na mwanamitindo huyo aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kuandaa mradi wa kijamii ambao ni sehemu ya shindano atakaloshiriki la taji la Dunia la Miss Journalism 2018 litakalofanyika Oktoba 27 Jijini Arusha.
Kufuatia uteuzi huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi kuandika barua ya uteuzi kwa balozi huyo mpya sambamba na kumkabidhi hati ya uteuzi ili pamoja na mambo mengine aweze kunadi vivutio vya utalii vya pori hilo.
Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara kuandaa safari maalum ya balozi huyo mteule aweze kutembelea Pori la Akiba Selous kwa ajili ya kuona na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu hifadhi hiyo kwa ajili ya utangazaji.
Sambamba na pori hilo atatembelea pia mapori mengine ikiwemo BBK (Burigi, Biharamulo na Kimisi) mkoani Kagera na Mpanga Kipengele mkoani Njombe ambapo atatumia fursa hiyo kufanya mahojiano na wasichana wa vijiji jirani na hifadhi hizo kwa ajili ya mradi wa kijamii wa kuwainua ikiwa ni sehemu yenye alama muhimu kwenye shindano hilo la Dunia la Miss Journalism 2018.
Awali akiwasilisha ombi lake kwa Waziri Kigwangalla la ufadhili wa safari yake ya ushiriki wa mashindano hayo, Witness pia aliomba kupewa fursa ya kuwa balozi wa Tanzania kwenye moja ya sekta ikiwemo Misitu, Nyuki au Utalii.
Mbali na kushikilia taji la Miss Journalism Tanzania 2018, Witness amesema amewahi kushinda mataji mengine manne makubwa ya kimataifa ya ulimbwende nchini Afrika ya Kusini anakosomea urubani kwa sasa.
Anasema, "Miongoni mwa mataji hayo ni Miss Garden Route 2017, ambalo ni taji la kitaifa la kuhamasisha na kukuza sekta ya Maliasili na Utalii nchini humo, licha ya kuwa ugenini nilitumia fursa hiyo kunadi vivutio vya utalii vya Tanzania.
"Mashindano haya yalihusisha washiriki 600 na wote walikuwa na asili ya kizungu, mimi peke yangu nilikuwa na asili ya kiafrika na niliibuka mshindi".
Aliyataja mataji mengine kuwa ni Miss Bees Cape Town 2017 kwa ajili kuhamasisha uhifadhi wa sekta ya nyuki na mataji mawili ya kimkoa ambayo ni Miss Asla Capetown 2017 na Miss Carnival Mosselbay 2017.
Mataji mengine ya kitaifa aliyowahi kushinda Witness hapa nchini ni pamoja na Miss Arusha Higher Learning 2014 na Miss Northern Zone 2014.
Mashindano hayo ya Dunia ya Miss Journalism 2018 yanahusisha pia uhamasishaji wa maendeleo ya utalii, utamaduni wa amani, uandishi wa habari na kupiga vita ugonjwa wa ukimwi na Malaria.
Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.