Kiongozi wa kundi la waasi la Allied democratic forces Jamil Mukulu, amefikishwa Mahakamani Kuu inayohusika na uhalifu wa kimataifa mjini Kampala, Uganda, Jumatatu miaka 3 baada ya kukamatwa nchini Tanzania.
Kikao cha mahakama cha jana Jumatatu kilikuwa cha kushauriana jinsi kesi dhidi ya Mukulu na wenzake 38 itaendeshwa.
Akiwa amefungwa pingu mikononi na minyororo miguuni, Jamil Mukulu na wenzake 38 walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa kikosi cha polisi cha kupambana na ugaidi.
Washukiwa hao waliendelea kufungwa pingu na minyororo hata baada ya kuwa tayari wako ndani ya mahakama hiyo.
Kwa mwongozo wa Jaji Eva Luswata, kikao cha jana Jumatatu kilikuwa cha kutoa fursa kwa wasimamizi wa mashtaka kuishawishi mahakama kwamba Jamil Mukulu na wenzake, wana kesi ya kujibu kuhusiana na ugaidi ndani ya Uganda.
Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kwamba kwa mda mrefu, tangu mwaka 1986, Mukulu, akiwa kiongozi wa kundi la allied democratic forces – ADF, alikuwa akisajili wapiganaji, kutekeleza mauaji, wizi wa kimabavu, kutoa mafunzo ya ugaidi na kutekeleza ugaidi, kujaribu kuua, kuteka nyara na kushirikiana na makundi mengine ya kigaidi kutekeleza mauaji katika nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Washukiwa wamefuatilia kikao cha mahakama kwa msaada wa wakalimani katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine asili kama lusoga, lugisu na Luganda.
Jamil Mukulu, anaripotiwa kupokea mafunzo ya moja kwa moja na aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama Bin Laden, upande wa mashtaka umeeleza.
Pia wamesema kuwa , mshukiwa huyu aliwahi kushiriki katika vita nchini Afghanistan. Video iliyotolewa na jeshi la Uganda UPDF inaonyesha kundi la ADF likiwa linafanya mazoezi katika misitu ya DRC kwa kutumia silaha nzito.
Mukulu alikamatwa mnamo mwaka 2015 akiwa nchini Tanzania kabla ya kurejeshwa nchini Uganda, ambako alikuwa akitafutwa kwa mda mrefu na kukwepa mitego ya maafisa wa usalama. Alifanikiwa kuhepa mitego ya maafisa wa usalama kwa kutumia majina bandia Zaidi ya 11 kwenye stakabadhi zake.
Alipokamatwa alipatikana na zaidi ya pasi za kusafiria 10 za nchi tofauti ikiwemo Uganda, Tanzania, Kenya na Uingereza.