LICHA ya kuanza vibaya kwa kuchapwa mabao 4-0 dhidi ya USM Alger katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali amefunguka kuwa kikosi hicho kijipange kuhakikisha kinavuka hatua hiyo ya makundi na kufika hatua ya robo fainali.
Yanga ikiwa ugenini katika mchezo wake wa makundi Kombe la Shirikisho ilikutana na kichapo cha mabao 4-0, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa July 5, 1962 nchini Algeria. Kwa matokeo hayo Yanga wanaofundishwa na Mkongomani Zahera Mwinyi wanashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa Kundi D.
Akizungumzia juu ya hilo, Akilimali alisema kikosi hicho kinatakiwa kujipanga vilivyo kuona kinapiga hatua na kufika mbele zaidi ya hatua hiyo ya makundi ambayo waliwahi kufika katika msimu wa 2015/16 ambapo walishiriki wakiwa wanafundishwa na Kocha Hans van Der Pluijm.
“Inshaallah Mwenyezi Mungu kama akijalia heri safari hii tunataka tuvuke hapa tulipofikia kama hatukufika nusu fainali basi tufike robo fainali na hilo ndilo lengo letu, Wanayanga tutazame tujipange sawasawa, kuhakikisha tunafika hatua hiyo,” alisema Akilimali.
Baada ya mchezo huo na USM Alger, kikosi hicho ya Yanga kinatarajia kujitupa tena uwanjani Mei 16, kucheza na Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa pili hatua ya makundi ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Kipigo cha Bao 4 Chamuibua Mzee Akilimali Atoa Neno Hili
May 09, 2018
Tags