Madee ni miongoni mwa mashabiki wa kutupwa wa Arsenal na mara kadhaa amekuwa akitoa maoni juu ya mwenendo wa klabu hiyo ikiwa ni pamoja na kutaka mzee Arsene Wenger kuachia nafasi ya ukocha.
Baada ya kuonekana mchezaji wa zamani wa Arsenal Mikel Arteta anapewa nafasi kubwa ya kuwa kocha wa klabu hiyo mkali wa BongoFleva Madee ametoa mtazamo wake juu ya Arteta kuwa kocha mkuu wa The Gunners.
“Kwa sababu tayari alikuwa pale Emirates North London, vitu vingi anavijua mule ndani, alitoka akaenda Manchester City kama kocha msaidizi tunajua Guardiola ni kocha mzuri kwa hiyo kuna vitu atakuwa kajifunza atavileta nyumbani, tunachoangalia na kusubiri ni kuona yale tunayoyatamani tutayapata?
“Hatutakiwi kuwa na matumaini kwamba tutapata mafanikio ambayo tunayaona kwa Zidane hiki ndio kitu kimewajaa sana mashabiki wa Arsenal.”
“Arteta sehemu ambayo yupo naamini ni sehemu ambayo anaifahamu vizuri na hatuna shaka nae kabisa.”
“Tutaanza kulalamika msimu wa 2019/20 lakini 2018/19 hatuta lalamika sana kwa sababu tutakuwa tunaangalia alichojifunza kwa sababu Arsenal ni timu kubwa na jukumu aliliopewa ni kubwa kuibeba Arsenal.”
“Nadhani kuna vitu vingi sana atatakiwa ajifunze kwa hiyo kwa msimu ujao mimi binafsi sitatoa lawama yoyote lakini 2019/20 nikiona bado tunaumia kama alivyokuwa Wenger itakuwa tatizo tena.”
“Sisi hatuhitaji sana wachezaji wa gharama kwa sababu hata falsafa yetu haituruhusu kwa hiyo hatuhitaji pesa za kununua wachezaji wa milioni 100, tunachohitaji ni beki wa kati na kiungo ndio maeneo yenye matatizo lakini mbele hatuna tatizo. Tunahitaji wachezaji kama watatu ‘world class’ lakini sio wa milioni 100 au 200.”