Sakata la kuzuiwa kwa meli mbili zenye tani 62,000 za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam, linatishia kuadimika kwa bidhaa hiyo baada ya viwanda vingi kusitisha uzalishaji.
Tayari bei ya mafuta ya kula imeanza kupanda kutokana na kuadimika kwake sokoni baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzizuia meli hizo tangu mwezi uliopita kushusha mzigo mpaka wamiliki wake watakapolipa kodi husika.
Utata wa kulipa kodi inayodaiwa na TRA, unatokana na madai ya mamlaka hiyo inayosema mafuta yaliyoingizwa ni safi ilhali wamiliki wakieleza ni ghafi.
Kwa utaratibu uliopo, mafuta safi ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya nchi hulipiwa kodi ya asilimia 25 wakati ghafi yanatozwa asilimia 10.
Licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi kulifuatilia suala hilo, mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo aliliambia Mwananchi kuwa hakuna namna zaidi ya wamiliki hao kulipa kodi husika badala ya kuendelea kulalamika.
“Ni kweli tunazishikilia meli mbili zenye mafuta ya kupikia. Wanachotakiwa ni kulipa kodi tu. Kama wanaona wameonewa wafuate utaratibu wa kukata rufaa, siyo kulalamika kwenye vyombo vya habari,” alisema Kayombo.
Hivi karibuni, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo bungeni jijini Dodoma, Majaliwa aliwahakikishia Watanzania kuwa bei ya sukari na mafuta ya kula hazitapanda kuelekea mfungo wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza Mei 15 kulingana na mwandamo wa mwezi.
Bei zinapanda
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwapo ongezeko la bei ya mafuta ya kupikia kuanzia mwishoni mwa Aprili. Mwananchi limeangalia bei hizo mpaka juzi jioni.
Jijini Arusha, lita moja imepanda kutoka Sh3,500 hadi 4,000 huku ndoo yenye ujazo wa lita 10 ikiuzwa Sh35,000 kutoka Sh31,000 za awali.
Jijini Dodoma, ndoo ya lita 20 ya mafuta hayo sasa inauzwa Sh70,000 kutoka Sh56,000.
Mkoani Geita, kibaba kilichokuwa kikiuzwa Sh100 sasa kinauzwa Sh300, wakati kibaba kimoja kinauzwa Sh500 kikiwa kimepanda kutoka Sh300 ya Januari jijini Mwanza.
Kwenye baadhi ya maduka jijini Dar es Salaam, robo lita imepanda kutoka Sh600 hadi Sh1,000, wakati nusu lita ikitoka Sh1,600 mpaka Sh2,000.
Lita moja iliyokuwa inauzwa Sh3,200 sasa ni Sh4,000 wakati ndoo ya lita 20 ikiuzwa Sh70,000 kutoka Sh55,000.
Kupanda kwa bei hiyo kunatokana na uwezo mdogo wa Tanzania kuzalisha mafuta ya kula. Takwimu za Chama cha Wasindikaji wa Mbegu za Alizeti (Tasupa), zinaonyesha mahitaji ya bidhaa hiyo nchini ni tani 570,000 kwa mwaka na wazalishaji wa ndani husindika tani 210,000.
Mwenyekiti wa Tasupa, Ringo Iringo anasema kati ya kiasi hicho kinachozalishwa nchini, tani 180,000 zinatokana na alizeti wakati vyanzo vingine ikiwamo pamba zikichangia tani 30,000 zilizobaki hivyo kulazimika kuagiza tani 200,000.
Tofauti na takwimu za mwenyekiti huyo, taarifa nyingine zinaonyesha mahitaji ya mafuta hayo ni tani 400,000, huku uzalishaji wa ndani ukiwa haufiki hata robo.
Mmoja wa wazalishaji wa alizeti anasema mbegu zote za alizeti zinazozalishwa nchini ni tani 100,000, zikikamuliwa hutoa tani 25,000 tu za mafuta ya kula.
Kati ya tani 80,000 za mbegu za pamba inayolimwa zaidi mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa mwaka, zikikamuliwa hutoa tani 10,000 za mafuta.
“Kwa takwimu hizi, uzalishaji wa ndani ni tani 35,000 za mafuta lakini bado Serikali inatoa kibali cha kuuzwa nje kiasi cha tani 10,000 kila mwaka. Kuzuiwa kwa mafuta hayo kunazidisha upungufu nchini,” kilisema chanzo kingine.
Mzozo
Wakati TRA ikiwataka waagizaji husika kulipa kodi inayodaiwa, kiongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Hussein Kamote alisema mabadiliko yanayoleta mkanganyiko unatokana na kanuni mpya za kodi zilizotungwa na mamlaka hiyo Februari, lakini zikitakiwa kutumika kuanzia mwishoni mwa mwaka jana.
“TRA wametunga kanuni Februari, lakini wanataka zianze kutumika kwa mizigo iliyoingizwa tangu Novemba mwaka jana. Pia, wanawataka wafanyabiashara walete nyaraka ambazo awali hawakuzidai,” alisema Kamote.
Kutokana na ugumu wa kupata nyaraka zinazohitajika, Kamote alisema itakuwa rahisi kwa TRA wakiziomba kutoka Serikali za nchi husika kwa sababu ni rahisi mamlaka za umma kubadilishana taarifa.
“Tunashangaa wanaposema ni mafuta safi wakati (Shirika la Viwango Tanzania) TBS, ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali na (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania) TFDA wameshakagua na kuthibitisha kuwa ni ghafi,” alisema Kamote.
Licha ya taasisi hizo kuthibitisha kuwa mafuta hayo ni ghafi, TRA imezitaka kampuni zilizoyaagiza kupeleka nyaraka kutoka Indonesia na Malaysia walikonunua ili kuthibitisha kama ni ghafi.
Kutokana na zuio la mafuta hayo ambayo ni malighafi kwa viwanda vya mafuta nchini vinavyojumuisha Bidco, East Coast, Azania na Murza Oil, vimelazimika kusitisha uzalishaji.
Mmoja wa wamiliki wa mafuta yaliyozuiwa bandarini alisema: “Hilo suala lina siasa ndani yake.”
Ofisa mmoja wa TBS ambaye aliomba kutotajwa, alisema suala hilo lipo ngazi za juu lakini tayari shirika hilo lilishayapima na kujiridhisha ni ghafi.
“TBS inatumia wataalamu, hatupimi kwa macho. Hilo suala tumeziachia Wizara za Fedha, Afya na Viwanda watalizungumzia wenyewe. Sisi tumepima na kuona ni mafuta ghafi, mkemia mkuu wa Serikali naye amekuta ni crude oil (ghafi), basi tumeziachia ngazi za juu,” alisema ofisa huyo.
Kaimu meneja masoko, mawasiliano na huduma kwa wateja wa ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali, Cletus Mnzava alitaka taarifa zitafutwe mamlaka nyingine.
“Ni vyema ukawauliza watu bandari kwa sababu wao wanajua nani aliyapima hayo mafuta. Kama ni vyakula kuna taasisi yake, kama ni kemikali kuna taasisi yake, ukiwauliza hao ndiyo wanajua,” alisema Mnzava.
Naye meneja mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Janet Ruzangi alisema mamlaka hiyo haihusiki na upimaji wa mizigo bali wenye jukumu hilo ni TRA.
“Kazi ya kupima ni ya TRA kwa sababu mizigo yote ikishafika bandarini huwa ni yao. Wakisema tupakue tunapakua, wakisema tuache tunaacha. Sisi tunatoa mizigo baada ya kuhakikisha nyaraka zote zimekamilika,” alisema Ruzangi.
Mkakati
Mwenyekiti wa Tasupa, Ringo Iringo alisema japo hawawezi kuziba pengo la mahitaji nchini, lakini wanaendelea kuongeza uzalishaji kuanzia kwenye kilimo hadi viwandani.
“Kwa Dodoma, mafuta ya Korie yamefikia Sh70,000 kwa ndoo ya lita 20 ila tunajitahidi kukamua mafuta ya kutosha ili kukidhi mahitaji. Mwaka huu wakulima wamevuna alizeti nyingi na ukamuaji umeongezeka, kwa hiyo tutapunguza tofauti ya mahitaji na uzalishaji uliopo,” alisema Ringo.
Vilevile, alisema Serikali imeimarisha uzalishaji wa pamba kwa kupeleka mbegu bora kuongeza uzalishaji wa mafuta.
Wiki iliyopita suala hilo liliibuka katika Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira mjini Dodoma, mwenyekiti wake Sadiq Murad alisema meli hizo zimekaa bandarini kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na ubishani kati ya Shirika la Viwango (TBS) linalosema mafuta hayo ni ghafi huku TRA ikipinga.