Magufuli Awataka Watendaji Idara za Maji, Ardhi Kuripoti Wizarani

Magufuli Awataka Watendaji Idara za Maji, Ardhi Kuripoti Wizarani
Rais John Magufuli ameagiza watendaji wa idara za maji na ardhi kuwajibika moja kwa moja Serikali Kuu kupitia wizara husika badala ya halmashauri.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, Ikulu jijini Dar es Salaam alipowaapisha balozi wa Tanzania nchini Cuba, Alphayo Kidata na katibu tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu. Hotuba yake ilitangazwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC1.

Alisema Serikali imewaacha watalaamu hao kwa muda mrefu wakitumia nafasi zao kuhujumu miradi ya umma, hatua inayochelewesha maendeleo ya wananchi na upatikanaji wa huduma za maji.

Rais alisema asilimia 75 ya miji wakazi wake wamejenga bila utaratibu wa mipango miji na changamoto hiyo imeendelea kuongezeka kutokana na udhaifu wa watendaji wa ardhi katika halmashauri.

Kuhusu changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maji, alisema kuanzia mwaka 2010 hadi sasa Serikali ina miradi yenye thamani ya Sh109 bilioni, lakini imetekelezwa kwa Sh17 bilioni.

“Wameleta miradi yenye thamani ya Sh109 bilioni, lakini value for money (thamani ya fedha) ya hiyo miradi mpaka leo kwamba kama kuna mradi unatakiwa kulipwa ni Sh17 bilioni, miradi inasomeka Sh109 bilioni, lakini thamani ya kazi zilizofanyika for ten years (kwa miaka kumi) ni Sh17 bilioni ambayo ndiyo inaweza ikalipwa, miradi mingine imekaa zaidi ya miaka minane haikamiliki,” alisema.

“Miradi mingine ni forgery (ya kughushi) tu, kinapelekwa kifaa tu na hayupo mtu wa kumbana kule kwa sababu hawa (Wizara ya Maji) hawako ‘connected’ (hawajaunganishwa) na watalaamu wenzao, sasa nimeamua wataalamu wote wanaohusika na maji kuanzia kwenye halmashauri watawajibika direct (moja kwa moja) na Wizara ya Maji ili injinia wa maji akifanya ujinga wilayani afukuzwe moja kwa moja na katibu mkuu.”

Rais alisema endapo wataalamu hao wakiendelea kusimamiwa na madiwani watabaki kuwa huru na changamoto hazitamalizika.

Pia, alimuagiza waziri wa wizara hiyo kutengeneza mabadiliko ya kimfumo ili kila bajeti ya maji itakapopelekwa katika halmashauri, waziri akasimamie mwenyewe na si halmashauri kama ilivyokuwa awali.

“Na katibu mkuu kiongozi kama kuna instruments (nyenzo) za kubadilisha, zibadilishe. Nataka hawa wasimamiwe moja kwa moja na wizara inayohusika, hatuwezi kupeleka miradi haitekelezwi. Hata wabunge wamezungumza sana kuhusu miradi kutotekelezwa yaani fedha inapelekwa lakini miradi hai-move (haiendelei) vizuri,” alisema.

Kama ilivyo katika sekta ya maji, Rais Magufuli alisema hali si nzuri katika sekta ya ardhi kwa wataalamu waliopo kwenye halmashauri mbalimbali.

“Maofisa ardhi, ma-planners, wataalamu wa mipango miji walioko kwenye halmashauri nao hawako answerable (hawawajibiki) wizarani, ‘connection’ haipo. Nakumbuka nikiwa waziri wa ardhi niliwaomba hawa watu, kwamba ‘nipeni niwanyoshe’ lakini nikakataliwa kwa sababu wana kiburi, wanatoa ‘double allocation’, wanafanya mambo ya hovyo hawashughulikiwi. Kwenye mkutano wa madiwani atazungumza hiki kinatakiwa hivi, anaweka na maneno ya Kiingereza madiwani wanaona huu ndiyo utaratibu,” alisema.

Alisisitiza kuwa katika vikao vya mabaraza ya madiwani wataalamu hao hufikia hatua ya kunukuu vipengele vya sheria zinazosimamiwa na wizara husika akitoa mfano wa zile zinazohusika na usimamizi wa ardhi.

Rais alisema wataalamu hao wako huru, wanafanya wanachotaka na hakuna wa kuwahoji na kuwawajibisha. Alitoa mfano wa utaratibu wa mwananchi kuomba kibali cha ujenzi akisema usumbufu unaotokana na mizunguko ya vikao kutumia muda mrefu imekuwa ikiwakatisha tamaa hatua inayochangia wajenge bila vibali. “Ukiwauliza wanasema kibali labda ukilipie, kikao kitakaa, wamekaa jana watakaa miezi miwili ijayo sasa umekopa benki unataka kuanza kujenga kesho, unasubiri kikao wakati mwingine kikao huko ukawape pesa, sasa hili nimeliona, nimepata malalamiko mengine ndiyo maana 75 ‘percent’ ya miji imejengwa kwenye unplanned areas (maeneo yasiyopangwa),” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa wataalamu hao pia wataanza kusimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Ardhi ili mtaalamu yeyote atakayeharibu afukuzwe siku hiyohiyo na katibu au waziri bila kusubiri kikao cha madiwani.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad