Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, amesema ameshangazwa na uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli kumteua kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM) kwa kuwa hakuwahi kuwaza kupata nafasi hiyo.
Makongoro ambaye ni mtoto wa nne kuzaliwa kwa Baba wa Taifa anakuwa wa kwanza katika familia hiyo kuwa mjumbe wa NEC.
Mwenyeti wa CCM, Rais Magufuli, jana alitangaza kuwateua Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere kuwa wajumbe NEC.
Makongoro amesema: “Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wangu wa chama amenishangaza kati ya nafasi zake zisizozidi saba za kuteua wajumbe wa NEC ameniteua na mimi.”
“Amenipa heshima kubwa sana kuniteua katika nafasi zake za kwanza tena na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ambaye ni kiongozi ninayemheshimu sana,” alisema Makongoro.
Alisema Rais Magufuli mara kwa mara amekuwa akitoa ahadi kwa Watanzania kuwa hatawaangusha katika utendaji kazi wake na hivyo kumteua kwake ni heshima kubwa.
“Si tu kunipa heshima bali pia ameona ninafaa na mimi naahidi sitamuangusha kwa sababu ameona namimi naweza kutoa mchango wangu katika vikao vya juu vya chama,” alisema.
Kuhusu uteuzi huo, Makongoro alisema hakuwa anafahamu jambo lolote na wala hakutarajia kupatiwa nafasi hiyo ya juu.
Alisema amekuwa akijishughulisha na kazi zake binafsi katika kipindi cha mwaka mmoja tangu akose nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki, mwaka jana.
“Nimekaa benchi kwa muda mrefu sasa na nimekuwa nikiendelea na shughuli zangu binafsi mkoani Morogoro huku nikiendelea kujifua na mazoezi kwa ajili ya kuwa mchezaji wa akiba” alisema huku akicheka.
Makongoro pia alisema neema ya uteuzi huo imekuja wakati ambao ni msimu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaowalazimu Waislam kote nchini kufunga ili kutimiza nguzo za dini hiyo.
“Kweli nimeamini mwezi Mtukufu wa Ramadhani upo, Nimeshuhudia Ramadhani nyingi wakati nasoma na hatua nyingine katika maisha yangu, lakini hii ya mwaka huu ni historia sitausahau mwezi huu mtukufu wa Ramadhani,” alisema Makongoro.
Kadhalika, Makongoro aliahidi kuwa mtumishi na mwanachama mwaminifu wa CCM na uadilifu mkubwa.
“Katika utumishi wangu kwa nafasi niliyoteuliwa ya mjumbe wa NEC nitakuwa mwadilifu kwa kuwasilisha matatizo ya wanachama na kuhakikisha yanasikilizwa na kufanyiwa kazi,” alisema Makongoro.
Aprili 24, mwaka huu, wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa benki ya NMB mkoani Dodoma, Makongoro alimwomba Rais Magufuli ampe kazi kwa sababu yeye ni mchezaji wa akiba akisubiri kuanza kazi.
Aliposimama kuzungumza kwenye tukio hilo, Rais Magufuli alisema Makongoro anastahili kuwa mchezaji wa nafasi ya kwanza na si mchezaji wa akiba.