Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa kwa siku tano kuanzia jana, ambazo zinaweza kuleta mafuriko katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika taarifa ya TMA iliyotolewa jana Mei 13, mvua hizo zilizoanza kunyesha zitaendelea mpaka Mei 17 mwaka huu.
TMA imesema athari zinazinaweza kutokea ikiwemo mafuriko ambayo yanaweza kusababisha kuvurugika kwa usafiri, barabara kubwa kutopitika na maisha ya watu kuwa hatarini kutokana na maji kujaa au kupita kwa kasi.
Pia imetoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zitakazotolewa.