Mbunge wa Viti MaalumuCCM), Mariamu Ditopile amesemaa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amemdanganya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu ununuzi wa tumbaku.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/19 bungeni leo Mei 15, 2018, amesema Dk Tizeba amemdanganya Majaliwa kwamba wanunuzi wa zao hilo walitaka kununua chini ya dola za kimarekani 0.8.
“Haujatusisimua (kwa bajeti yake) nothing (hakuna kitu), utashi wako upelekee kukua kwa uchumi wa viwanda lakini wewe ndiyo unavuruga.
Wanunuzi wanataka kununua Tumbaku kwa dola 1.3 (za kimarekani) lakini wewe unakataa, ukamlisha tango pori waziri mkuu,”amesema.
Amesema ukweli ni kwamba wanunuzi hao walitaka kununua tumbaku kwa Dola 1.3 ya Marekani lakini waziri wa kilimo alikataa bei hiyo na matokeo yake akasababisha hasara kwa wakulima.
“Wale wakulima hawana vihenge, mvua iliponyesha tumbaku yao ilinyeshewa na mvua matokeo yake wamekuja kuuza chini ya dola 0.8 ya Marekani walichokipata walitumia kulipa madeni,”amesema.
Akizungumzia zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, Mariamu amesema: “Mheshimiwa waziri wewe ni swahiba wangu lakini uswahiba wangu hauuzidi wa wakulima. Najua wakulima wanavyotoa jasho na machungu wanayoyapata. Mahindi tunalima kwa ajili ya chakula na biashara. Tumezalisha kwa zaidi ya asilimia 120.”
Hata hivyo, amesema wakulima hao wamekosa soko la mahindi baada ya Serikali kuzuia uuzaji wa mahindi nje ya nchi na kwamba yeye ni mmoja wa waadhirika ambaye amelazimika kuyatupa mahindi baada ya kukosa soko.
Mariamu amesema kuwa wizara hiyo imeleta miche ya mikorosho mkoani Dodoma lakini hakuna mafunzo yaliyotolewa kwa maofisa ugani wala wakulima na kushauri ni vyema Serikali ikawa na mpango wa mazao wa kikanda.
Amesema pia, waziri huyo amekuwa akiwachanganga wakulima kwa kusema kuwa dawa ya kuulia wadudu ya sulpher itatolewa bure kwa wakulima wa korosho lakini baadaye anawataka kulipia.
“Mliombwa mtoe bure? Waliwaambia shida yao ni sulpher? Ghana wameweka mpango baada ya miaka 10 watakuwa wakizalisha korosho ya kutosha. Sisi tunampango wa kulifanya zao hili kuwa endelevu?”amehoji.
Amesema iwapo zao hilo la korosho mkoani Dodoma litastawi kwa asilimia 10 atajiuzulu ubunge.