Mbunge wa Kibiti Ally Ungando ameitaka serikali kutatua suala la maji jimboni kwake kwani yeye kama Mbunge wa Jimbo hilo amechoka kusuluhisha migogoro ya ndoa inayotokana na uhaba wa maji.
Akichangia hoja Bungeni Mbunge amesema kwamba tatizo hilo la maji linawafanya kina mama wengi kuamka alfajiri na kwenda mbali kutafuta maji, huku wakichukua muda mrefu na kuwafanya waume zao kukosa imani nao wakiamini huenda wanachepuka kwa wengine, na kusabaisha migogoro ya mara kwa mara.
“Kule jimboni kwangu nimechoka kusuluhisha ndoa kwa sababu ya muda mwingi wanandoa wanakwenda kutafuta maji visimani, baba anashindwa kuwa na imani mkewe amekwenda kisimani au amekwenda kwa mchepuko, kwa sababu maji yanatoka mbali, na ukienda yanakuwa ya kulindia, kwa hiyo baba anakosa imani, kwa hiyo tumekuwa na migogoro mikubwa ya wanandoa kule kwangu Kibiti, kwa hiyo Mheshimiwa angalia na kule Kibiti kwa jicho la huruma tuweze kutatuliwa tatizo la maji”, amesema Mbunge huyo.
Sambamba na hilo Mbunge amesema kwamba jimboni kwake kuna miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa licha ya kuwa karibu na mto Rufiji, lakini inashangaza kukosa maji kwa ajili ya wananchi wake mpaka sasa.