Mbunge wa Mlimba kupitia CHADEMA Suzan Kiwanga ameitaka serikali kupitia waziri wa elimu Joyce Ndalichako, kuendelea na mfumo wa kukaririsha madarasa wanafunzi kwani bila kufanya hivyo inasababisha wanafunzi wengi kutohitimu na kukosa elimu.
Suzan Kiwanga ameyasema hayo Bungeni ambapo pia amemtaka Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako kuliangalia hili kwa undani zaidi, kwani waathirika wakubwa ni watoto wa kike, pale wanaposhindwa kufaulu mtihani na kuendelea nakidato cha tatu, hivyo hulazimika kuolewa wakiwa na umri mdogo kwa kuwa wanakosa cha kufanya.
“Sasa kukariri hamna, watoto ni wasichana, Ndalichako na wewe mwenyewe ni mwanamke, watoto wasichana wasipokariri waende wakaolewe!? Wakiwa bado wadogo!? Mi naona acheni watoto waendelee kusoma wakue shuleni wapate elimu baadaye hata wakitupwa huko mbali kama ataolewa yeye au atalima yeye”, amesema Mheshimiwa Kiwanga.
Licha ya hilo Mbunge Kiwanga ameitaka seikali kuangalia na utungaji wa mitihani, kwani kuna utofauti mkubwa wa ubora wa elimu wanaopata wanafunzi wanaoishi mazingira ya mjini, na wale wanaoishi vijijini kwani wengi wao hawana walimu.