Mbunge wa Kilombero kwa tiketi ya CHADEMA Mhe. Peter Lijualikali amemwomba Rais Magufuli kuangalia uwezekano wa kuwarejeshea wakazi wa Kilombero eneo la ardhi kubwa inayomilikiwa na watu wachache na kusema kuwa anaamini leo ataondoka na watu hao ambao wamekuwa wakihodhi maeneo hayo makubwa
Lijualikali amesema hayo leo Mei 4, 2018 mbele ya Rais Magufuli kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi katika Barabara ya Kidatu Ifakara mkoani Morogoro, na kudai kuwa atashukuru kama Mhe. Rais atafanya maamuzi hayo na kudai pasipo kufanya hivyo hata hiyo barabara itakayojengwa itakuwa haina maana.
"Ukiniambia leo uwape zawadi gani watu wa Morogoro maana kuna mengi lakini naomba watu wote ambao wamechukua ardhi yetu na hawaifanyii kazi basi naomba leo uondoke nao kwa sababu watu hao wanahujumu rasilimali yetu na hii barabara kama tutaacha hivi basi kwetu itakuwa haina faida na mimi kama Mbunge nilikuwa nawaambia wananchi wangu msiuze ardhi hovyo kwani ardhi ndiyo rasilimali yetu"
Aidha Mbunge Lijualikali amemuomba Rais Magufuli asaidie katika kuweka sawa uhusiano kati ya wananchi wa Morogoro na wamiliki wa kiwanda cha sukari cha Kilombero na kudai pamoja na kuwa kinazalisha ila uhusiano wa kiwanda hicho na wananchi.
"Wananchi wana shida ya kujua wingi wa sukari, wanashida ya kujua ni namna gani uzito wa mua unapatikana kwani kiwanda ndiyo kinapima chenyewe uzito, kiwanda kinapima chenyewe wingi wa sukari wananchi wanapewa tu hesabu sasa hatuwezi kujua tunaibiwa au tuko sahihi"