Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Mohamed Abood ameiomba Serikali kutumia ramani ya mwaka 1970 kuwapatia haki yao ya ardhi wananchi wa Kata ya Kauzeni na Luhogo mkoani Morogoro ambao maeneo yao yameingiliwa na mipaka ya kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Abood ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Mei 30, 2018 wakati akiuliza swali la nyongeza kufuatia majibu ya Serikali kuwa wananchi wa eneo hilo hawana mgogoro na JWTZ baada ya upimaji wa mwaka 2002.
“Wananchi wa maeneo hayo walianza kuishi hapo mwaka 1969 na ilipofika mwaka 1970 Serikali iliwapimia eneo hilo lakini cha kushangaza kila wakati wanaambiwa wamevamia ni kwa nini mipaka ya mwaka 1970 isitumike ili wabaki na maeneo yao,” amehoji Abood.
Katika swali lake la msingi, mbunge huyo amesema ni lini Serikali itawarudishia wananchi maeneo yao ya kilimo, kuhoji kwanini isichukue hatua kwa kuruhusu wananchi wamiliki maeneo hayo kwa kuwa JWTZ imewakuta.
Katika majibu yake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi amesema ufumbuzi wa mgogoro wa mipaka ulishafanyika kwa kushirikiana na halmashauri ya Manispaa ya Morogoro hivyo jeshi halina mgogoro na wananchi wa maeneo hayo.
Amesema manung’uniko yaliyopo yanatokana na uamuzi wa JWTZ kusitisha utaratibu wa kuwaruhusu kwa muda baadhi ya wananchi kulima mashamba ndani ya mipaka yake kwa sababu za kiulinzi na usalama.
“Haitakuwa vyema kwa JWTZ kuondoka katika maeneo yaliyochaguliwa kistratejia za ulinzi, kuondoka katika maeneo haya kutaligharimu Taifa hivyo wananchi waelimishwe juu ya jambo hili,” amesema Mwinyi.